NA MWANAJUMA MMANGA

JESHI la polisi Mkoa Mjini Magharibi limesema linawashikilia watu 72 wanaohusishwa na kufanya ghasia katika kipindi cha uchaguzi uliomalizika hivi karibuni.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Madema.

Alisema watu hao wanahusishwa na kufanya uvunjaji wa sheria ikiwemo kuweka mawe barabarani, na kuchoma matairi katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Aidha, Kamanda Awadh, alisema kufanya hivyo ni kitendo cha uvunjifu wa Amani, jambo ambalo ni kosa la kisheria.

Alisema jeshi la polisi linaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha amani na utulivu unadumu nchini na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa wanaochochea kuhamasisha vurugu kufuata njia za kisheria kuwasilisha malalamiko yao.

“Kitendo cha uvunjifu wa amani hakileti taswira nzuri katika kuharibu amani iliyotawala na  kuvuruga nchi “ alisema.

Hivyo amewasihi wananchi kutojiingiza katika uvunjifu wa sheria, kwani jeshi hilo liko imara kuhakikisha wanawachukulia hatuwa wavunjifu wa sheria.

Hata hivyo, amewataka wananchi wasijiingeze katika vitendo vya kihalifu na kwamba yeyote atakaebainika kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani hatuwa za kisheria zitachukuliwa dhidi yake