MWANASAYANSI wa China aliyesaidia nchi mbili zenye nguvu zaidi duniani kufika kwenye mwezi, lakini sasa anatambulika katika nchi moja tu. Nini kilichotokea?

Huko Shanghai kuna makumbusho yenye bidhaa za kale 70,000 ambazo zote ni za mtu mmoja tu aliyejulikana kama, “Mwanasayansi wa watu” Qian Xuesen.

Qian ndie mwanzilishi wa mradi wa makombora ya anga za juu nchini China, ambapo utafiti wake ulisaidia ubunifu wa roketi ambazo ziliwezesha China kupeleka Setelaiti ya kwanza kwenye anga la mbali.

Makombora hayo yalikuwa ni sehemu ya silaha za nyuklia, hivyo mwanzilishi huyo anachukuliwa kama shujaa wa taifa.

Lakini katika nchi nyingine zenye nguvu zaidi duniani, ambako amesomea na kufanya kazi kwa mwoyo mmoja, mchango wake hautambuliki kabisa.

Qian baada ya kuonesha kipaji chake hapo awali, alitunukiwa ufadhili wa masomo katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts Marekani.

Qian alizaliwa mwaka 1911, wakati utawala wa kifalme wa China ulikuwa unakaribia kubadilika na kuwa wa Jamhuri.

Baada ya kuhitimu chuo cha Massachusetts aliingia chuo chengine cha Teknolojia cha California, aliposoma na mwanasayansi maarufu duniani Theodore von Karman.

Pia aliwahi kuwa ofisi moja na mwanasanyansi mwingine mashuhuri Frank Malina.

Kuna siku ambayo Qian alijikuta kwenye mjadala wa mahesabu na Bwana Malina kuhusu utafiti wa namna ya kusukuma roketi.

Lakini wakati huo hakuna aliyechukulia mazungumzo hayo kwa uzito hadi kulipotokea vita vya pili vya dunia.

Hivyo wanasayansi hao walilivutia jeshi la Marekani ambalo liliwapa pesa ili kufanya utafiti wa kusaidia ndege kupaa na vifaa vya kuwezesha hilo viliwekwa kwenye mbawa za ndege ili kuziwezesha kupata hewa kwenye barabara ya ndege.

Qian alipewa cheti cha mtafiti wa silaha na kupewa kazi katika serikali ya Marekani kama mshauri wa Bodi ya Sayansi.

Na hadi wakati vita vya pili vya dunia vinamalizika alikuwa miongoni mwa wataalamu maarufu kwenye masuala ya ndege na aliagizwa pamoja na Theodore von Karman kwenye ujumbe maalum Ujerumani lengo likiwa ni kupeleleza wahandisi waKinazi.

Lakini kufikia mwisho wa kazi hiyo taaluma ya Qian iliyokuwa iking’aa, ilizima ghafla pale China na Marekani zilipoanza kuwa maadui.

“Manamo mwaka 1949, Mwenyekiti Mao wa nchini China alitangaza kuundwa kwa Jamhuri ya Kikomunisti, na mara moja sana Marekani ikaichukulia China kama adui”, alisema Chris Jespersen.

Hivyo akachaguliwa mkurugenzi mpya katika oparesheni za ndege, ambaye aliamini kwamba kuna watu wanaofanya upelelezi katika maabara yao huko Marekani.

Wakati vita baridi vinaendelea, ndipo Shirika la Ujasusi la Marekani lilipodai kuwa Qian na wanasayansi kama Frank Malina na wengine wa Kikomunisti ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani.

Makosa aliofunguliwa Qian ni pamoja na kuonesha kuwa alihudhuria mkutano uliodhaniwa kuwa wa chama cha China cha Kikomunisti, ingawa alikanusha madai hayo na kusema yeye sio mwanachama.

Hata hivyo, utafiti mpya ulionesha kwamba alijiunga na chama hicho wakati mmoja na Frank Malina mnamo mwaka 1938.

Zuoyue Wang, profesa wa historia wa chuo kikuu cha Ufundi cha California, Pomona, anasema hakuna ushahidi ulioonesha kwamba Qian aliwahi kufanya upelelezi kwa ajili ya China ama alikuwa afisa wa kiintelijensia alipokuwa Marekani.

Hata hivyo alipokonywa leseni yake na kuhukumiwa kifungo cha nyumbani, huku wanasayansi wenzake akiwemo Theodore von Karman waliandikia serikali kuomba Qian aachiliwe huru kwasababu hakuwa na hatia, lakini hakuna aliyesikiliza ombi hilo.

Mwaka 1955, wakati Qian alikuwa ametumikia kifungo cha nyumbani kwa miaka mitano, Rais Eisenhower alifanya maamuzi ya kumfurusha nchini humo na kumrejesha kwao China kwa lazima.

Hatimae mwanasayansi huyo aliondoka Marekani kwa kutumia boti akiwa na mke wake pamoja na watoto wake wawili waliozaliwa Marekani.

Wakati akiondoka aliwaambia wanahabari kwamba hatawahi kurejea tena Marekani na mwanasayansi huyo alitimiza ahadi yake.

“Alikuwa miongoni mwa wanasayansi maarufu sana Marekani. Alikuwa amechangia pakubwa katika nchi hiyo kimaendeleo ya kisayansi na pia kuna uwezekano mkubwa angeifanyia Marekani uvumbuzi wa ajabu, kwa hiyo sio tu kwamba ilimdhalilisha lakini pia ilimsaliti,” alisema mwanahabari na mwandishi, Tianyu Fang.

Alipofikia China, Qian alipokewa kama shujaa, lakini hakujumuishwa moja kwa moja kwenye chama cha Kikomunisti.

Na alipojiunga na chama hicho rasmi mwaka 1958, alijitahidi sana kutoenda kinyume na utawala uliokuwepo, na hatimae alifanikiwa kujiendeleza katika taaluma yake.

Wakati anawasili China kulikuwa na uelewa mdogo kuhusu masuala ya sayansi ya roketi, lakini miaka 15 baadae aliongoza uzinduzi wa satelaiti ya kwanza ya China kwenda kwenye anga za mbali.