NA EMMANUEL MBATILO

Utazamaji wa Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani kupitia Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia nchini (REDET) ulionesha kuwa kwa ujumla kampeni za Uchaguzi zilifanyika katika mazingira ya utulivu na amani kukiwa na matukio machache ya vurugu.

Akizungumza na Wandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa REDET, Prof. Rwekeza Mukandala, amesema Chama Cha Mapinduzi CCM na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA walifanya mikutano mingi zaidi ya Kampeni kuliko vyama vingine na njia za usafiri zilizotumika zikiwa ni magari ambapo CCM ilikuwa na misafara ya magari makubwa yaliyopakwa rangi ya kijani.

Aidha Prof. Mukandala amesema Mgombea Urais wa CHADEMA naye pia alikuwa na msafara wa magari kadhaa wakati akisaka Kura na ilipofika mwisho wa kampeni CCM na CHADEMA walitangaza kuwa wataanza kutumia usafiri wa helikopta ili kufikia maeneo mengi zaidi kwa muda mfupi.

“Kulikuwa na ratiba iliyokubaliwa na wagombea wote na vyama vyote viliifuata. Hata hivyo, baadhi ya vyama vya siasa havikuonekana kabisa katika maeneo waliyoainisha na kwa muda uliowekwa.

Pamoja na hayo, Prof. Mukandala amesema katika mikutano ya kampeni ya Uchaguzi ya wagombea Urais walionekana askari polisi wa kutosha na kwa ujumla REDET ilitazama mikutano 5131 ya kampeni za uchaguzi  na kati yake mikutano 1385 sawa na asilimia 27 ndio ilikuwa na askari polisi waliovalia sare.

Sambamba na hayo Prof. Mukandala, amesema REDET ilitazama mikutano 5131 na 466 kati yake asilimia tisa iliendelea zaidi ya saa 12 jioni. Pamoja na ukiukwaji huu wa sheria na taratibu polisi walikuwa wavumilivu na hivyo kuzuia uwezekano wa mivutano.

“Katika matukio 75 ya uvunjifu wa taratibu yaliyoshuhudiwa na REDET ni matukio sita yaliyohusisha polisi kuzuia kufanyika kwa mikutano ya kampeni”. Amesema Prof.Mukandala.