KHAMISUU ABDALLAH NA HAFSA GOLO 

SHANGWE, vifijo na nderemo zilitawala kila kona ya kiwanja cha Amani kufuatia kuapishwa na kukabidhiwa madaraka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi.

Hayo yalibainika wakati wa tukio la kihistoria la kukabidhiana madaraka ya kiti cha urais ambapo ipo kisheria kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

Majira ya saa 1:00 asubuhi kiwanja cha Amani kilisheheni umati wa watu waliovaa rangi ya kijani kibichi, njano na bluu huku wengine wakivaa suti za rangi ya bluu na nyeusi ikiwa ni utamaduni wa mzanzibari.

Aidha hali hiyo ilikuwa pamoja na shamrashamra na nyuso za tabasamu kwa wananchi hao huku muziki, bendi na taraabu zikiendelea kuleta burudani kiwanjani hapo.

Katika majira ya saa 4:02 asubuhi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliwasili kiwanjani hapo na kupokewa na viongozi wa madhebu mbalimbali ya dini, majaji, wazee na viongozi wengine wa serikali hadi jukwaa kuu la kiapo.

Dk. Hussein Mwinyi alikaa hapo kwa muda wa dakika 13 kumsubiri Rais wa Zanzibar wa awamu ya saba, Dk. Ali Mohamed Shein ili zoezi la kula kiapo liendelee.

Mara baada ya kuwasili Dk. Ali Mohamed Shein majira ya saa 4:24 ilipigwa mizinga 21 sambamba, kushushwa bendera ya rais na gwaride la kuagwa serikali ya awamu ya saba lilinguruma uwanjani likijumuisha vikosi vya Jeshi la Wananchi, Polisi, JKU, Mafunzo, Valantia, KMKM.

Kitendo hicho kilikuwa pamoja na helkopta ya kizita iliyotoka kaskazini kuelekea Kusini ikiashiria kitendo cha kumuaga Rais wa awamu ya saba, Dk. Ali Mohamed Shein zoezi ambalo lilikwenda sambamba na ushushwaji wa bendera ya rais kwa awamu hiyo.

Aidha mnamo majira ya saa 4:32 ukimya uliwatawala kiwanjani hapo kwa dakika chache ambapo bila shaka iliashiria kumbukumbu za uongozi mahiri wa Dk. Shein katika kuwatumikia wananchi wa visiwa vya Zanzibar na kubaki sauti za vyombo vya matumbuizo ikiwemo bendi ya polisi.

Hali hiyo pia ilijitokeza kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali ambapo wengine nyuso zao zilionesha huzuni na simanzi wakati akiwaaga na kuwapungia mikono akiwa katika gari la wazi.

Hata hivyo katika majira ya saa 4:48 zoezi la kiapo cha kukabidhiwa matakwa ya kikatiba kwa rais wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi kilichukua nafasi yake ambapo kiongozi huyo alionekana katika nyuso ya tabasamu na nguo maridadi alizovaa zenye rangi nyeusi na tai nyekundu.

Baada ya zoezi hilo kukamilika nyimbo za asili na tamaduni za mzanzibari ziliimbwa katika majukwaa mbalimbali kiwanjani hapo.

Mara baada ya kusita kwa kitendo hicho viongozi wa madhehebu mbalimbali walimuombea dua ili aweze kuongoza nchi kwa kufuata misingi ya sheria na kuepuka mambo ambayo hayana msingi kitendo kilichochukua takriban dakika saba.

Aidha kukamilika kwa kiapo hicho Rais Mwinyi alisalimiana na viongozi wote waliokuwepo jukwaa kuu la kiapo na majira ya saa 5:12 alipanda jukwaa maalum lililoandaliwa kwa ajili ya kupewa heshima na kupandishwa bendera ya rais wa serikali ya awamu ya nane huku akipigiwa mizinga 21 na nyimbo za taifa zikiimbwa ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi uongozi wake.

Baadae zilitolewa salamu za jeshi kwa umbo la ALFA kwa ajili ya kumkaribisha huku ilipofika 5:19, Dk. Mwinyi alikagua gwaride lililoongozwa na kamanda wa gwaride kanalI Donald Matutu Sengo na baadae kupanda jukwaa kuu lililokuwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.

Katika majira ya saa 5:35 kikosi cha jeshi kilipita mbele ya Rais wakifatiwa na ndege tatu zenye maana ya kuashiria suala la ulinzi wa anga katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake sambamba na ndege moja kubwa ya salamu ya heshima.

Aidha 5:37 gwaride lilitoka uwanjani na wananchi waliendelea na vifijo, nderemo na vigeregere kuashiria kusubiri hotuba nzito iliyojaa maslahi na wazanzibari.