HATIMAYE mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 umemalizika, baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kumtangaza Dk. Hussein Mwinyi kuwa Zanzibar na kushukua nafasi ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Mwinyi anakuwa rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa awamu ya nane, tangu visiwa hivi vilipolazimika kuuondoka ukoloni wa kisultani mnamo mwaka 1964.

Dk. Mwinyi alikuwa mgombea anayetoka Chama cha Mapinduzi, alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 380,402 ambazo ni sawa na asilimia 76.27, akimshinda mshindani wake mwanasiasa mashuhuri Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.

Kama wazanzibari, kwanza tunapaswa kuinua mikono kuomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu mola muumba wetu kwa kutuwezesha kulimaliza zoezi la mwaka huu kwa amani.

Bila shaka yoyote mchakato wa uchaguzi hapa Zanzibar, ulikuwa miongoni mwa mitihani ama majaribio ya namna gani tumekomaa katika kuiendeleza na kuitunza amani.

Kutokana na kuufaulu vizuri mtihani huo, tunaweza kusema kuwa wananchi wa Zanzibar wameingia kwenye mkondo wa ukomavu uliotokana na kutumia njia za busara za utatuzi wa changamoto hiyo iliyokuwa ikitukabili.

Wakati tukishukuru kwa Mwenyezi Mungu kwa kulimaliza zoezi hilo kwa njia ya amani, huu ni wakati wa kuja pamoja kama wananchi wa Zanzibar kusahau tofauti zetu za kisiasa na kuendelea na maisha yetu ya kawaida.

Tunasema hivyo hasa ikizingatiwa kuwa sisi wazanzibari sote ni ndugu wa damu, ni ndugu wa dini, wazanzibari ni watu wenye utamaduni mmoja, hivyo kubakia na vinyongo na mafundo rohani si jambo kufanyiana ndugu kwa ndugu.

Lazima tukubali na tuamini kwenye nyoyo zetu kwamba mchakato wowote wa uchaguzi hutoa mshindi mmoja, na mtu huyo anapotangazwa na kulishwa kiapo cha uongozi anakuwa kiongozi wa wananchi wote.

Kwa maana hiyo kama walivyo viongozi wengine waliomtangulia katika awamu zilizopita, Dk. Mwinyi atakuwa rais wa wananchi wote wa Zanzibar na si rais wa Chama cha Mapinduzi na wanachama wa chama hicho pekee.