BEIJING,CHINA

RAIS Xi Jinping wa China amesema nchi yake huenda ikakuza maradufu uchumi wake na kuwa taifa lenye mapato makubwa kufikia mwaka 2035.

Shirika la habari la Xinhua linaloendeshwa na serikali ya nchi hiyo, limeripoti kwamba Rais Xi alisema hayo juma lililopita alipoelezea sera mpya za miaka mitano na za muda mrefu wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Shirika hilo lilibainisha kwamba Rais Xi alitaja athari hasi za janga la virusi vya corona kwa taifa hilo,lakini akasema China ilichukua hatua za ufufuaji uchumi kwa haraka zaidi kuliko nchi nyengine duniani.

Shirika la Xinhua lilisema Xi anataraji Pato Ghafi la ndani la Nchi kwa mwaka huu kukua kwa hadi yuan trilioni 100 ama takribani dola trilioni 15.

Liliripoti kuwa Xi alisema hatua za upande mmoja na za kujilinda zinadhoofisha mzunguko wa uchumi duniani,ikiwa ni bayana ni shutuma aliyoielekezea Marekani.

Pia aliripotiwa kusema kwamba China inapaswa kulenga kuweka msingi wa maendeleo yake ndani ya nchi.