NI jambo la kusikitisha sana kuiona sehemu kubwa ya jamii ya Zanzibar inayoelezwa kuwa ina waislamu zaidi ya asilimia 90, lakini kila kukicha kuna taarifa za ongezeko kubwa la talaka.

Takwimu za miaka mitatu iliyopita, zilibainisha kwamba kwa mwezi mmoja Zanzibar kuna wastani wa talaka kati ya 80 hadi 100, ambapo ukichukulia hesabu hiyo kwa mwaka utabaini kwamba kuna idadi kubwa ya watu wanaopoteza ndoa zao.

Kinachoshangaza ni kwamba ndoa nyingi zinazovunjika ni za vijana wa chini ya umri wa miaka 30, huku wengine baadhi yao wakivunja ndoa bila ya kutimiza hata mwaka mmoja.

Tunakubali kama mafundisho ya dini yanavyotueleza kwamba talaka ni halali, lakini Mwenyezi Mungu anaichukia, hata hivyo ameruhusu watu kuachana endapo kuna ulazima wa kuvunjwa kwa ndoa hiyo.

Bila shaka kuna sababu nyingi za ndoa changa kuvunjika hapa visiwani, hata hivyo sababu kubwa zaidi ni kwa wanandoa wengi wakiwemo hao vijana hawana elimu ndoa.

Kuna huzuni kubwa katika jamii ndoa ilizofungwa kwa misingi ya uislamu, lakini wakati wa kuachana hawafuati utaribu wa jinsi ya kuihalalisha hiyo talaka.

Kwa mfano ziku hizi mume akiacha mke humfukuza mbio aende kwao, wakati sheria inaeleza kama talaka hiyo ni ya kwanza ama ya pili mke ana haki ya kukaa kwenye nyumba hiyo hadi eda ishe.

Wakati wa talaka sheria zote huwekwa pembeni siku ya pili fuso liko uwanjanoi tayari kuhamisha makabati na vitanda, si hasha gari hilo lililoletwa kubeba mizigo ya mke linashindikizwa kwa beni ili watu wajue kuwa fulani kaachwa.

Mafundisho hayo pia yanatueleza kuwa mke anapoachwa wakati hajamaliza eda mume ana haki ya kumlisha na kumpa matunzo. Haya yote ambayo yapo kwenye sheria yanakiukwa.

Ndoa zimekosa misingi, wanandoa hawana uvimilivu, wanandoa wameshindwa kuwa na ustahamilivu, katika nyumba mume mkali kama kisu mke naye hashikiki kama mto kila mtu amejaa jazba.

Watu wengi hufikiri kupeana talaka ndio njia ya kumaliza matatizo, uzoefu unaonesha kwamba kuachana ndio chanzo cha matatizo kwani huishia watoto kukosa matunzo hadi kupelekana kwenye vyombo vya sheria.

Tunaipongeza sana Ofisi ya Mufti wa Zanzibar ambayo baada ya kuliona tatizo la kutamalaki talaka katika jamii, wamechukua hatua ya kuweka chuo maalum cha mafunzo ya ndoa.

Tunafiri chuo hichi kinaweza kuwa msaada mkubwa katika kunusuru kuvunjika kwa ndoa katika jamii, kwani tatizo kubwa ni kwamba wanandoa hukurupuka kufunga ndoa bila ya kuwa na elimu ya ndoa.

Bila shaka katika mafunzo hayo wanandoa hufunzwa misingi, sheria za ndoa, hufunzwa namna ya kukaa na kuishi vyema na mwenza wako, hufunzwa, uvumilivu na ustahamilivu na kadhalika.

Wapo wanaodhani chuo hicho ni kwa wale waliokuwa hajaoa ama kuolewa, hapana hata kama umeoa ama umeolewa mafunzo ya chuo hicho yanakufaa kwani yatakusaidia kuishi kwneye ndoa yako na yatakuongoza kila ulipokuwa unakosea.

Tunadhani ifike wakati wenye kutaka kufunga ndoa wasifungishe ndoa bila ya kuwa na cheti cha kupitia mafunzo ya ndoa kama vile ilivyo hivi sasa hufungi ndoa kama hujapima UKIMWI.