ANKARA,UTURUKI

VIKOSI vya huduma za dharura bado vinaendelea na shughuli za utafutaji na uokoaji nchini Uturuki na Ugiriki siku tatu baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea katika bahari ya Aegean.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.0 kwenye kipimo cha Ritcher na tsunami iliyofuata vilitokea Ijumaa iliyopita katika bahari ya Aegean inayopatikana kati ya Uturuki na Ugiriki.

Mamlaka za Uturuki zinasema watu wasiopungua 98 walifariki na 994 kujeruhiwa nchini humo,ikiwa za Ugiriki imethibitisha vifo viwili na majeruhi 19 kutokana na janga hilo.

Katika jimbo lililoathiriwa zaidi la Izmir magharibi mwa Uturuki, jitihada kubwa zinaendelea za kuwatafuta na kuwaokoa manusura kwenye majengo yaliyobomoka katika maeneo matano hata baada ya saa 72 muhimu kupita.

Mamlaka zimewaelekeza wakaazi kuhama majengo yanayoweza kubomoka.

Watu kadhaa wanaishi katika zaidi ya makaazi ya muda 3,000 yaliyotengenezwa kwa mahema.

Waendesha mashitaka wa Izmir waliwakamata watu tisa waliohusika katika ujenzi na uidhinishaji wa majengo yaliyobomoka.

Wanawahoji ikiwa walizingatia viwango vya kuhimili matetemeko ya ardhi katika ujenzi wa majengo hayo.