NA MWANAJUMA MMANGA

UMOJA wa Vyama vya siasa Zanzibar umewahimiza wananchi kuendelea na harakati za kujenga nchi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu hivi karibuni.

Aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa vyama vyao vimekubaliana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi Zanzibar na kuahidi kumuunga mkono Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyeapishwa kushika wadhifa huo baada ya kutangazwa mshindi.

Viongozi hao walieleza hayo katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni mjini Unguja na kwamba kinachohitajika kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa aliyechaguliwa kuiendeleza Zanzibar   kimaendeleo.

Ameir aliwataka wananchi kuepuka kukaa vikundi na kuamini kuwa uchaguzi utarejewa kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

“Uchaguzi umekwisha kinachotakiwa hivi sasa kujenga mashirikiano ya pamoja baina ya wananchi na viongozi wa siasa na Rais aliyechguliwa kuijenga Zanzibar na kuleta maendeleo,” alisema ameir ambae pia ni Katibu wa chama hicho.

Kwa upande wake Hamad Mohammed Ibrahim aliyekuwa akiwania nafasi hiyo kupitia chama cha UPDP alisisitiza haja ya wananchi kumuunga mkono Dk. Mwinyi kwa kuwa amechaguliwa na Wazanzibari walio wengi.

Alifafanua kuwa miongoni mwa wagombea 17 walioteuliwa kuwania wadhifa huo walikuwa na nafasi sawa katika ushindani hivyo uamuzi wa wananchi uheshimiwe.

Aidha alipongeza hotuba ya Dk. Mwinyi aliyoitoa juzi baada ya kula kiapo akiamini kuwa ana wajibu wa kuwatumikia bila kubagua itikadi zao za chama hivyo kutokana na jambo ambalo litasaidia kuimarisha umoja na maelewano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.

Naye Naibu Katibu wa Chama cha TLP ambae aligombea urais kupitia chama hicho, Hussein Juma Salum, aliwaomba wananchi kushirikiana na Dk. Mwinyi ili kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo.

Kauli ya viongozi wa umoja huo unaoundwa na vyama ADA TADEA, SAU, CCK, UPDP, NRA, DP, Demokrasia Makini, NLD na TLP, imekuja siku moja baada ya kuapishwa kwa Dk. Mwinyi na kuahidi kutoa mchango na kuhakikisha nchi inaimarisha uchumi wake.