NAIROBI,KENYA

WAKILI mmoja wa Kenya amejisalimisha kwa viongozi wa Uholanzi ili kukabiliana na mashitaka dhidi yake kwenye Mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC).

Wakili huyo anadaiwa kuwahonga mashahidi katika kesi dhidi makamu rais wa Kenya William Ruto katika Mahakama hiyo.

Wakili Paul Gicheru alikuwa anatafutwa na warranti ya ICC tangu mwaka wa 2015, akishtumiwa kujaribu kuwapa hongo mashahidi sita wa muendesha mashitaka ili wabadili Ushahidi wao katika kesi dhidi ya William Ruto.

Ruto na mwanahabari Joshua Sang, walishitakiwa kwa kuchochea ghasia za kikabila baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2007 ambapo watu elfu 1,200 waliuwawa.

Mwaka 2016, majaji waliamuru kwamba hakuna kesi yoyote ya kufuatilia, licha ya kuwa walitoa nafasi ya kupokea mashitaka mapya, wakihisi kwamba kesi hiyo ilidhoofishwa na muingilio wa siasa na vitisho dhidi ya mashahidi.

Kulingana na shirika la habari la Reuters, msemaji wa Ruto hakupendelea kutoa maelezo yoyote kuhusu kesi ya wakili Gicheru, lakini alisisitiza kwamba Gicheru hakuwahi kufanya kazi kama wakili wa Ruto.

Reuters haikufanikiwa kumpata muakilishi wa Gicheru.

Katika taarifa,ICC iliwaomba viongozi wa Uholanzi kumfikisha mahakamani Gicheru, mara tu utaratibu wa kumkamata utakapomalizika.

Kesi nyengine inayodai kuhusika kwa rais Uhuru Kenyatta katika ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ilipingwa na mahakama hiyo mwaka 2015.