Yumo kiongozi muandamizi wa ACT-Wazalendo

NA HAFSA GOLO

JESHI la Polisi Zanzibar, limethibitisha kumshikilia naibu katibu mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Nassor Ahmed Mazuri na wanachama wengine 34 kwa tuhuma za kutaka ‘kudukua’ matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Bomani mjini Zanzibar, Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mohammed Haji Hassan, alisema wamefanikiwa kumkamata Mazuri na idadi hiyo ya watu wengine wakiwa katika moja ya chumba katika hoteli ya Mazsons wakiingilia matokeo ya uchaguzi.

Chama hicho kimekuwa kikieleza katika vyombo vya habari kwamba hawafamu wapi kiongozi wao huyo alipo.

“Tumewakamata baada ya kupokea taarifa kuna kukindi cha watu chenye mipango ya kuingilia matokeo ya uchaguzi mkuu, hivyo taarifa hiyo tuliifanyiakazi”, alisema.

Kamishana huyo alisema baada ya kufanyiwa upekuzi katika chumba kimoja wapo katika hoteli hiyo na kuwakuta na wakiwa na vifaa kadhaa walivyokuwa wakivitumia kuingilia matokeo ya uchaguzi.

Alivitaja vifaa walivyokamatwa navyo ni pamoja na kompyuta (laptop) 34, Ipads, simu, nyaraka mbalimbali zenye matokeo ya uchaguzi mkuu na vifaa vyengine walivyokuwa wakivitumia kuingilia matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema miongoni mwa waliokamatwa wamo wanawake wawili, ambapo alibainisha kuwa upelelezi unaendelea na utakapokamilika hatua kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Katika hatua nyengine Kamishna huyo alisema kwamba mnamo Oktoba 28 mwaka huu majira ya saa 6 usiku, jeshi hilo lilipata taarifa kuwepo watu waliopewa mabomu.

Alisema watu hao waliingiza mabomu hao ili wayatumie kuripua sehemu mbalimbali hapa Zanzibar, ambapo baada ya kuifanyia kazi taarifa hiyo, walifanikiwa kumkamata kijana mmoja aliyekuwemo kwenye mpango huo.

Alisema katika mahojiano alieleza mabomu alipewa katika hoteli ya Mazsons na kueleza kuwa pia wapo watu wengine katika hoteli hiyo waliopewa mabomu hayo ambapo wanaendelea kuwatafuta.

“Ndugu wananchi tunawataka muwe watulivu wakati upelelezi unaendelea na msijiingize katika vitendo vya uhalifu na yeyote atakayejaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani hatua stahiki dhidi yao zitachukuliwa”, alisema Kamishna.

Katika hatua nyengine Kamishna huyo alisema mwenyekiti wa ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad amefunguliwa jalada ambapo na yupo nje kwa dhamana.

Kuhusu maandamano ya upinzani yaliyopangwa kufanywa hapo kesho, alisema jeshi hilo lina taarifa kamili za mpango huo, hata hivyo limeonya kwamba maandamano hayo lazima yafuate sheria.

“Tunazo taarifa za kuwepo maandamano kesho tarehe 2, lakini maandamano hayo lazima yafuate sheria”, alisema Kamishna huyo.