NA MADINA ISSA

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imefanya uteuzi wa wanafunzi wapya 1,900 kwa ngazi za shahada ya kwanza ya pili na ya tatu, ili kuweza kujiendeleza kimasomo katika vyuo vilivyokuwepo Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa bodi hiyo, Iddi Khamis Haji, alisema pamoja na uteuzi huo wa wanafunzi wapya, lakini pia bodi hiyo inaendelea na ufadhili kwa wanafunzi 3,020 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbali mbali

Alisema kwa awamu hiyo ya mwanzo wanafunzi walioteuliwa ni 1,594 ambapo ni sawa na asilimia 70 kwa maombi yaliyokamilika ambapo nafasi zilizosalia zitajazwa mwishoni mwa mwezi wa Novemba wakiwemo wanafunzi wa vyuo vya nje

Aidha, alifahamisha kuwa katika nafasi hizo za ufadhili hakutakuwa na nafasi za vyuo vya nje kwa fani, ambazo zinapatikana nchini ambapo umuhimu wa fani za nje utakuwa kwa fani adimu ikiwemo udaktari wa wanyama, udaktari bingwa na fani ya mafuta na gesi

Akizungumza kuhusiana na nafasi 100 za ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizotangazwa kama zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwa kidato cha sita, alisema wanafunzi hao watalipiwa ada ya masomo na mitihani kwa asilimia 100, posho ya kula na kulala na gharama za mafunzo ya vitendo

Hivyo, alisema jumla ya gharama zitakazotumika kwa wanafunzi wote wakiwemo wapya na wanaoendelea na masomo katika vyuo ni shilingi bilioni 12.8 kwa wanafunzi 4,920

Aidha alifahamisha kuwa bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni 12 kwa wanafunzi wote ambao ni 4,920 wakiwemo wanaoendelea na masomo 3,020 na wanafunzi wapya watakaoteuliwa ambao ni 1 900.

Alisema kuwa jumla ya maombi yaliyotolewa ni 2786 ikiwemo ya shahada ya kwanza, 2,640 shahada ya pili 128 na shahada ya tatu 17, ambapo maombi yaliyokamilika yalikuwa ni 2,429 sawa na asilimia 90 ya maombi yaliotumwa.