PARIS,UFARANSA

SKULI  zote nchini Ufaransa zinamuenzi mwalimu aliyeuawa baada ya kuwaonesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Muhammad.

Wanafunzi walirejea skuli baada ya mapumziko ya msimu wa pukutizi.

Wao pamoja na walimu walikaa kimya kwa muda ili kumkumbuka Samuel Paty aliyetumia vibonzo wakati wa darasa lililohusu uhuru wa kujieleza.

Mwalimu mmoja katika skuli ya sekondari ya chini mjini Paris aliwaambia wanafunzi wake kwamba ni muhimu kulinda uhuru wa kujieleza ulioenziwa kwa muda mrefu nchini humo.

Kufuatia mauaji ya mwalimu huyo, Rais Emmanuel Macron aliahidi kutoikatia tamaa haki ya raia kuonesha vibonzo.

Hata hivyo msimamo wake uliibua hasira kutoka kwa Waislamu.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alisema daima angetetea uhuru wa kujieleza lakini uhuru huo si ule usio na ukomo.