Na Mwantanga Ame

TANZANIA imemaliza uchaguzi wake Mkuu ambapo sasa inatafuta viongozi wa watakaoshika madaraka katika nafasi mbali mbali za kuiongoza nchi.

Nafasi zitakazojazwa ni pomoja na teuzi zitakazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi na nyengine zitahusu vyama vya siasa ambao wataounda serikali.

Kwa mantiki hiyo basi, hivi sasa kutakuwa na uchaguzi wa kuwania nafasi mbali mbali zikiwemo za Umeya na Uspika wa Baraza la Wawakilishi na Bunge.

Imezoeleka mara nyingi nafasi hizi kuona wanaojitokeza zaidi ni wanaume, kama vile na wanawake hawana haki ya kuwania nafasi hizo, kwa vile inaonekana sio mazoea yao.

Ushahidi wa hilo, Meya wa kwanza wa Zanzibar alikuwa ni Marehemu Mtoro Rehani Kingo, na kufuatiwa na Mrembo, Johari Yussuf Akida,  Maulid Salum Kibanzi,  Ahmeid Keis, Khatib Abdurahman, Mahboub Juma na marehemu Mjaka.  

Inafurahisha kuona mwaka huu, katika chaguzi za kutafuta nafasi ya Urais kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano kuna wanawake waliojitokeza kuwania nafasi hizo, ambapo kwa Zanzibar walifikia watano na Tanzania bara ni wawili.

Wagombea hao wameonesha umahiri wa hali ya juu kwamba wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi, kwani kitendo chao cha kuthubutu waliuthibitishia umma kwamba wanaweza.

Kutokana na hilo ipo haja ya kuliangalia eneo la Umeya linalohitaji kufanyiwa kazi kwa wale waliopitishwa kuwa Madiwani katika majimbo mbali mbali ya Unguja na Pemba ama Tanzania nzima, kwani ndani ya miaka 56 tangu Mapinduzi kufanyika kwa Zanzibar ni mwanamke mmoja tuu aliyewahi kuwa Meya, ambaye alikuwa Johari Yussuf Akida.

Kutokana na kuwa tayari imezoeleka nafasi za Umeya basi wagombea wake ni wanaume tuu, huku kukiwa na wanawake ambao wanauwezo mkubwa wa kuifanya kazi hiyo.

Baya zaidi, wanawake hao wamekuwa ni sehemu ya kuwafanyia kampeni Madiwani hao wanaume, huku wakiwapigia vigeregere baada ya kushinda katika chaguzi zao za Umeya.

Nafikiri sasa imefika wakati wa kubadilika kwa Madiwani wanawake waliochaguliwa katika uchaguzi wa vyama vyao, na kuona umuhimu wa kugombea tena nafasi za juu ndani ya Mabaraza ya Madiwani, ili kuleta mlingano utaonesha uwepo wa mabadiliko katika chombo hicho.

Inawezekana ikawa zipo sababu mbali mbali ikiwemo ile ya wingi wa idadi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kuwa ni wanaume wanaoongoza kuliko wanawake, lakini hicho kisiwe kigezo cha kushindwa kutumia nafasi hizo kwa kujitokeza kuwania Umeya.

Ni Dhahiri kuwa bado nguvu ya mwanamke iko kubwa kiushawishi kiasi ambacho sasa imefika wakati wa kuona umuhimu wa kuitumia bila ya kujali yale mambo yaliozoeleka ya kutupiwa kashfa ama matusi ya nguoni.

Hili linapaswa kulizingatia, kwani hivi sasa mnatakiwa kujali zaidi namna ya kutumia sheria ambazo zipo na zinafanyakazi zake pindi mkifikwa na matatizo ya aina hiyo.

Hivyo basi, ipo haja mkaaza kuona umuhimu wa kuwania nafasi hizo, ili muwe wa kwanza kwa Zanzibar kuendeleza  kuwa na Meya Mwanamke, kwa vile historia nyingi zinazoipamba dunia zipo zilizoanzia Zanzibar.

Itapendeza kwa mwaka huu, Chama kilichofanikiwa kupeleka wajumbe wengi wa CCM ndani ya Baraza la Madiwani, likaliona hili na kulifanyia kazi kwa dhati,  kwani hakuna lisilowezekana.

Nasema hivi sio kwamba nina nia ya kuwaharibia wale walioanza kutia nia ya kutaka kuwania nafasi hizo hasa wanaume, lakini nafikiri umefika wakati hivi sasa kwa kuwakumbusha wanawake kuona umuhimu wa kuwapa nafasi kuendesha shughuli za majiji.

Inawezekana wapo ambao wataona wazo langu liko kinyume na mtazamo wao hasa wanaume, lakini huo ndio ukweli kwamba imeshafika wakati sasa wa kuona umuhimu wa kubadilika, kwani miaka yote tangu Mapinduzi ya 1964, walipewa nafasi hiyo ni wanaume na wanawake walibakia kuwa wasindikizaji.

Hivyo basi, umefika wakati wa kufanya historia ijirejee, kwa kujitokeza kuwania Umeya na kuwapa nafasi wanawake washike uongozi huo, ili vigezo vya utendaji uonekane uwezo wao, kwani hakuna lisilowezekana.