KAMPALA,UGANDA

POLISI nchini Uganda wamesema kwamba watu 16 wamefariki na 65 kujeruhiwa kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu Bobi wine.

Msemaji wa polisi jijini Kampala Patrick Onyango alisema kwamba zaidi ya watu 350 walikamatwa.

Viongozi wa chama cha Bobi Wine walisema kwamba polisi walikataa mtu yoyote kuonana naye anapozuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya mjini Jinja, mashariki mwa Uganda.

Nalufenya ni kituo cha polisi chenye historia ya ukandamizaji mkubwa wa haki za kibinadamu,ambapo washukiwa wa makosa makubwa kama ugaidi huzuiliwa.

Barabara kuingia katika tija mji mkuu Kampala zilifungwa huku idadi kubwa ya polisi na wanajeshi wakishika doria.

Waziri wa habari alitoa taarifa inayomsifu Rais Yoweri Museveni, namna anavyokabiliana na waandamanaji na kutoa wito kwa raia kuwatambua watu wanaofanya vurugu, kuwakamata na kuwapeleka polisi.

Msemaji wa polisi Patrick Onyango,alisema kwamba waliokamatwa walikuwa wanaharibu mali,wizi, kuchochea ghasia,kuwapiga polisi mawe na kushiriki maandamano kinyume cha sheria.

Wagombea kadhaa wa urais kupitia vyama vya upinzani walisitisha kampeni zao hadi Bobi Wine atakapoachiliwa huru.

Uchaguzi wa Uganda umepangwa kufanyika Januari 14 mwaka ujao 2021.