TATU MAKAME NA MADINA ISSA

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamemchagua Zubeir Ali Maulid wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Spika wa Baraza la 10 la wawakilishi Zanzibar lililoanza kazi jana.

Zubeir aliechaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo katika baraza la tisa baada ya kumshinda pandu ameir kificho, katika uchaguzi wa jana aliibuka mshindi baada ya kupata kura 70 ambazo ni aslimia 100 ya kura halali.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Katibu wa Baraza hilo, Raya Issa Msellem alisema zubeir aliwashinda Ali Makame Issa wa chama cha wananchi (CUF), Naima Hamad Mohemed wa UDP, Ameir Hassan Ameir wa Demokrasia Makini na Hamad Mohamed Ibrahim wa UPDP ambao hawakupata kura.

Mkutano huo ambao ulianza saa 8:00 mchana kwa katibu huyo kusoma tangazo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kama inavyoelekezwa na katiba ya zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha mkutano huo pia ulitanguliwa na dua kabla ya wajumbe wateule kupiga kura za kuchaguza spika ambapo wagomea wote walipata nafasi ya kujieleza na kuomba kura ambapo pamoja na mambo mengine, wagombea hao waliahidi kuimarisha umoja na mshikamano wa wajumbe na vyombo vyengine.

Aidha wagombea hao waliahidi kuimarisha maslahi ya wajumbe pamoja na kuimarisha hadhi ya chombo hicho chenye wajibu wa kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Baada ya kuchaguliwa na kula kiapo cha uamionifu mbele ya katibu wa baraza hilo, aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua na kuahidi kufanya kazi kwa umakini na uweledi.

“Kura nilizopata kwa kweli mumenikopesha imani kubwa na ninaahidi kukulipeni kwa kuwatumikia kwa uaminifu kama mlivyoonesha uaminifu kwangu,” alisema Zubeir na kukishikuru Chama cha Mapinduzi kwa kumteua kugombea nafasi hiyo.

Aidha spika huyo alianza kazi kwa kuwaapisha wajumbe hao kutoka majimboni, viti maalum wanawake, wa kuteuliwa na Rais na Mwanasheria Mkuu wa serikali huku wajumbe wanne kutoka chama cha ACT Wazalendo wakishindwa kufika kula kiapo.

Baraza hilo limeakhirishwa hadi Novemba 10 saa nane mchana ambapo pamoja na kazi nyengine, baraza hilo litachagua naibu spika wa baraza atakaesaidiana na spika kuendesha vikao vya baraza hilo ambalo linaundwa na vyama vya CCM na ACT Wazalendo.