NA MWANAJUMA MMANGA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini unguja Ayoub Mohammed Mahmoud, amewataka madereva wa gari ya mchanga kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa na serikali ili kuzuia uchimbaji wa mchanga kiholela.

Alisema serikali imeweka utaratibu wa kukata kibali maalumu kwa ajili ya uchimbaji na upakiaji wa mchanga ili kuzuia uchimbaji wa mchanga kiholela na kuzuia uharibifu wa mazingira. 

Mkuu wa Mkoa huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akikabidhi gari lililokamatwa kwa kosa la kupakia mchanga kinyume na utaratibu huko kituo cha polisi Mkokotoni.

Ayoub aliahidi kuwachukulia hatua za kisheria madereva wote ambao watakwenda kinyume na utaratibu uliowekwa na serikali ili kuzuia vitendo hivyo.

Hata hivyo aliliagiza jeshi la polisi katika mkoa huo, kuacha tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa madereva wanaofikishwa katika vituo vya polisi na badala yake wasimamie sheria ili kudhibiti vitendo vya kihalifu visiendelee kutokea katika jamii.

Alisema alifahamu uwepo wa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuchimba mchanga kwa kutumia magari ya ng’ombe badala ya magari makubwa jambo linalopaswa kudhibitiwa. 

Alifahamisha kuwa kazi kubwa ya jeshi la polisi ni kusimamia usalama wa raia na mali zao pamoja na kutenda haki kwa wananchi hivyo ni busara kwa askari kuzingatia sheria na utaratibu wa kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hata hivyo Ayoub aliliagiza jeshi hilo kufanya doria za mara kwa Mara ili kuweza kuwafichua wahalifu ambao wamekuwa wakirudisha nyuma juhudi za serikali katika kupeleka mbele gurudumu la maendeleo.

Mapema akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Mkoa, askari wa kituo cha polisi Mkokotoni Sajenti Makame Bakari, alisema gari hiyo imekamatwa kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wananchi pamoja na jeshi hilo.

Aliitaja gari hiyo yenye namba za usajili Z413LF ambayo dereva wake hakupatikana, imefikishwa katika kituo cha polisi mkokotoni kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.