NA AMEIR KHALID, DAR ES SALAAM

MASHINDANO ya nane ya taifa ya ‘Baseball na Softball’ yamefunguliwa jana katika skuli ya viwanja Azania jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo Ofisa Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, Adolf Ally, aliipongeza Zanzibar kwa kufanya vyema katika michezo mbali mbali.

Alisema Zanzibar imekuwa ikifanya vyema katika mashindano inayoshiriki, hivyo amewataka kuendelea kujitahidi kufanya vyema ili kuzidi kupata sifa zaidi.

Adolf amewataka washiriki wa mashindano hayo kuhakikisha wanacheza kwa bidii na nidhamu pamoja na kuonyesha vipaji vyao ili kuchaguliwa katika timu za taifa, na kupata mafanikio zaidi.

Naye Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Hassan Khairalla Tawakal, alisema michezo ni moja ya eneo kubwa linalowaunganisha Watanzania.

Adha alivipongeza vyema vya michezo vya TaBSA na ZaBSA kwa mashirikiano makubwa wanayoyaonyesha katika kuendesha michezo hiyo, na kuwaomba waendelee kushirikiana.

Mapema Katibu wa TaBSA, Alfred Nchimbi, akitoa taarifa ya mashindano hayo alisema huu ni mwaka wa nane tangu kuanza mashindano, ambayo yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi mkubwa.

Alizitaja timu zinazoshiriki mashindano hayo ni wenyeji Azania ‘A’ na ‘B’, Zanzibar, Sanya Juu, Juhudi, Hondoro, Kibwegele, Kibamba na Kibaha.