NA MWANAJUMA MMANGA

MTU mmoja amefariki dunia na mwengine kujeruhiwa baada ya ajali ya gari kuacha njia na kumgonga mwenda kwa miguu huko Jambiani Mbuyuni, Wilaya ya Kusini Unguja.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa huo Suleiman Hassan Suleiman, alimtaja marehemu huyo kuwa Jamila Haji Bati (7) mkaazi wa Jambiani.

Kamanda Suleiman alisema tukio hilo limetokea Disemba 18 mwaka huu majira ya kiasi cha saa 2:30 asubuhi huko Jambiani Mbuyuni.

Alisema kuwa kijana Abubakar Abdalla Abdalla (27) mkaazi wa Jambiani Mbuyuni alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota priveti namba Z.494 KX iliyokuwa ikitokea Shungi kuelekea Paje amemgonga mwenda kwa miguu aliyekuwa akikatisha barabara kutokea upande wa kushoto na kumsababishia maumivu kichwani na kukimbizwa hospitali ya Makunduchi ambako alifariki dunia.

Alisema mara baada ya uchunguzi wa daktari na kupigwa picha na polisi mwili wa marehemu huyo ulikabidhiwa na jamaa zake kwa ajili ya mazishi na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva huyo na kusababisha kifo kwa marehemu huyo.

Hivyo kamanda alitoa wito kwa madereva kuwa waangalifu pale wanapokuwa barabarani ili kuepusha ajali zisizokuwa za ulazima.

Wakati huo huo watu wasiojulikana wamefanikiwa kuiba mbuzi sita na kuwachinga hapo hapo huko Binguni Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Kamanda wa polisi mkoa huo Suleiman Hassana Suleimna alisema tukio hilo limetokea mnamo Desemba 11 mwaka huu majira ya saa 8:12 za ausiku huko Binguni.

Alisema vijaa hao waliiba mbuzi hao majike walikuwa watano na dume mmoja wote wakiwa na tahamani ya shilingi 650,000 ambao mali ya Said Abdalla Yussuf (52), mkaazi wa Binguni.

Kamanda Suleimna alisema mbuzi hao walichinjwa hapo hapo na kuchukua nyama yote na kubakisha vichwa tu.

Aidha alisema mwenye mbuzi hao huwa wana kawaida ya kuwalaza nyumbani kwake bandani lakini ilipofika asubuhi anakwenda bandani hakuna mbuzi hata mmoja kitu ambacho kinasikitisha.

Suleiman alisema wizi wa mifugo katika wilaya yake umeshamiri siku hadi siku, hivyo amewaomba vijana wenye tabia kama hiyo kuacha nan a tabia kama hiyo wakijua kuwa ni kosa la kisheria.