NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA ya mkoa Mwera, imemuhukumu kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka minane mshitakiwa Mussa Ameir Khamis (35) mkaazi wa Jambiani wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Said Hemed Khalfan, mara baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo, ambae anadaiwa kubaka na kutorosha.

Akitoa ufafanuzi juu ya adhabu hizo, Hakimu huyo alisema kwa kosa la kubaka atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitano na kutorosha atumikie miaka mitatu.

Huku akifahamisha kuwa, adhabu kwa mshitakiwa ziende tofauti na haki ya rufaa imetolewa kwa upande uliokuwa haujarudhika na adhabu hizo.

Pia alisema mshitakiwa huyo amlipe fidia muathirika (victim) fedha taslimu shilingi 2,000,000 ili iwe fundisho kwake na wenziwe wenye tabia kama hizo.

Kesi hiyo ilifunguliwa Novemba 5 mwaka jana na kuanza kusiklizwa ushahidi Novemba 19 mwaka huo huo na jumla ya mashahidi watano walithibisha makosa hayo.

Mapema wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor, alisema kitendo alichofanya mshitakiwa huyo si cha kiungwa kwa kumuingilia mtoto wa miaka mitano.

Hivyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali pamoja na kumlipa fidia mtoto huyo kwa sababu tayari amemuharibia maisha yake yote kwa ujumla.

Mussa anadaiwa kutenda kosa la kubaka mnamo mwezi Febuari 2 mwaka 2015 majira ya saa 11:45 za jioni huko Jambiani Miuli wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa alimuingili kimwili mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano (Jina linahifadhiwa na gazeti hili) huku akijua kuwa ni kosa kisheria.

Aidha mshitakiwa huyo mnamo Febuati 3 mwaka 2015 majira ya saa 11:45 za jioni, alimchukua mtoto huyo aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake kutoka nyumbani kwao na kumpeleka katika boma la nyumba huko huko Jambiani, bila ya ridhaa ya wazazi wake.