NA TATU MAKAME
MTU mmoja anaekisiwa kuwa na umri wa miaka (24) mkaazi wa Mbuzini Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, amenusurika kufa baada ya kujaribu kujiua kwa kunywa vidonge aina ya vivian kwa kinachodaiwa kukataliwa na mpenzi wake.
Akizungumza na gazeti hili shuhuda wa tukio hilo aliyejitabulisha kwa jina la Khamis Nkale Masalago mkaazi wa Mbuzini alisema tukio hilo lilitokea Disemba 21 mwaka huu, majira ya saa 15:30 mchana Mbuzini.
Alisema kijana huyo wa kiume (jina linahifadhiwa) alijaribu kujiua kwa kumeza vidonge kumi na kupoteza fahamu kutokana na wivu wa mapenzi baada ya kukataliwa na mpenzi wake (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka (21) mkaazi wa Mbuzini.
Hata hivyo shuhuda huyo alieleza kuwa majeruhi kabla ya kuchukua uamuzi huo alikwenda nyumbani kwa jirani yake ambae ni mama mkwe wake anakoishi aliyekuwa mke wake na kumtaka warejeane.
Hata hivyo baada ya kutaka ridhaa hiyo mtalaka huyo alikataa na kusema hayuko tayari kurejea kwa aliyekuwa mumewe.
Aidha shuhuda huyo alieleza kuwa baada ya hatua hiyo majeruhi huyo aliacha ujumbe wa kuashiria kuhatarisha maisha yake kwa kudai kuwa bora afariki kuliko kukataliwa na mpenzi wake huyo kutokana na kuishi nae kwa muda wa miaka miwili akiwa ni mke wake wa ndoa na baadae kuachana.
Hata hivyo baada ya nasaha hizo kijana huyo aliingia ndani ya nyumba ya mama mkwe wake na kunywa vidonge na kupoteza fahamu.
Alieleza kuwa baada ya tukio hilo majeruhi alikimbizwa Hospitali ya KMKM kwa matibabu kabla kupelekwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu zaidi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadhi Juma Haji, alisema alipokea taarifa za kijana huyo kunywa sumu baada ya kukataliwa na mpenzi wake.
Hata hivyo alisema majeruhi anaendelea na matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja na hali yake inaendelea vizuri.
Kuhusiana na tukio hilo Kamanda Awadhi, aliwataka wananchi kuacha kuchukua maamuzi magumu ya kutaka kujiuwa kwa sababu ya kukataliwa kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.