NA TATU MAKAME

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, linamshikilia Ali Ramadhani Amour (31) mkaazi wa Nungwi kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.

Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo , Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Haji Abdalla Haji, alisema tukio hilo lilitokea Disemba 19, mwaka huu, majira ya saa 7:2 mchana huko Nungwi Wilaya ya Kaskazini ‘A’.

Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alipatikana na dawa hizo baada ya kupekuliwa na Polisi baada ya msako uliofanywa na jeshi hilo la kupamba ana watumiaji, wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya mkoani humo.

Alisema siku hiyo mtuhumiwa huyo alipatikana na  unga unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya  aina ya heroin vifurushi vitano vyenye uzito  wa grams  2.35 vikiwa vimehifadhiwa kwenye  mfuko wa suruali aliyokuwa amevaa.

Alisema kabla mtuhumiwa kutiwa mikononi, polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kijana huyo anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, kikosi cha kupambana na dawa za kulevya walifanikiwa kumfanyia upekuzi na kufanikiwa kumkuta na kiwango hicho.

Hata Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani taratibu zitakapokamilika na sasa yupo chini ya ulinzi kwa hatua za kisheria.

Kuhusiana na tukio hilo Kamanda huyo ameendelea kuwatahadharisha vijana kujiepusha na biashara ya dawa za kulevya, ili kujiepusha na matatizo.

Nao wananchi wa mkoa huo walilitaka jeshi la polisi kumchukulia hatua kali mtuhimiwa kwani si mara ya kwanza kupatikana na dawa za kulevya.