NA HUSNA SHEHA

KESI ya kijana aliyejiondoshea uaminifu baada ya kuaminiwa, inatarajiwa kuanza kusikilizwa ushahidi katika mahakama ya Mkoa Mahonda.

Kesi hiyo inayomkabili kijana Ame Sheha Pili (50) mkaazi wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, alifikishwa mahakamani hapo wiki mbili zilizopita, mbele ya Hakimu Makame Khamis.

Akiwa mahakamani hapo, mshitakiwa huyo alisomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Khamis Othman.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo inaeleza kuwa, Julai 25 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alidaiwa kuwa mshitakiwa huyo aliaminiwa kwa kupewa ng’ombe dume mwenye rangi nyekundu mali ya Ahmed Mjaka Hamad, mwenye thamani ya shilingi 105,0000 kwa lengo la kumuuza na kisha kurejesha fedha hizo na kushindwa kurejeshea kama walivyokubaliana, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hata hivyo upande wa mashitaka ulidai kwamba, kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 254 (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Mshitakiwa huyo baada ya kusomewa shitaka lake alikataa huku upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika na kuiomba mahakama impangie tarehe nyengine.