NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya mwanzo Mwanakwerekwe chini ya Hakimu Nassem Faki Mfaume, imemuhukumu mshitakiwa Mwana Fetu Sadik (30) mkaazi wa Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kulipa faini ya shilingi 100,000 na fidia ya kima kama hicho kwa malamikaji.

Mahakama ilitoa adhabu hiyo, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo dhidi ya shitaka lilokuwa likimkabili mshitakiwa huyo, ambapo jumla ya mashahidi watano walitoa ushahidi wao akiwemo askari na mpelelezi.

Hakimu Nassem alisema, mshitakiwa huyo akishindwa kulipa faini hiyo atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitano na kutoa haki ya rufaa kwa siku 30 kwa mtu asieridhika na hukumu hiyo.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.

Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai, alidai kuwa upande wa mashitaka umeshamaliza kuwasilisha mashahidi na mshitakiwa huyo ameshajitetea mahakamani hapo.

Mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la shambulio la kuumiza mwili, kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 25 mwaka huu na Mwendesha Mashitaka, Sajenti wa Polisi Hassan Mussa Mshamba, mshitakiwa huyo alimshambulia Halima Nassor Msanif, kwa kumpiga kifimbo cha kusukumia chapati sehemu ya kichwani na kumtafuta kidole cha shahada mkono wa kulia, na kumsababishia maumivu makali jambo ambalo ni kosa kisheria.