NA MWANDISHI WETU

MWANANCHI mmoja anayemiliki ardhi huko Buyu wilaya ya Magharibi ‘B’, Said Abrahman Juma, ameelezea kusikitishwa na uvamizi uliofaywa kwenye eneo lake na kukatwa viwanja bila ya kushirikishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema, eneo hilo analimiliki baada ya kulinunua na kupatiwa uhalali wa kulimiliki kutoka familia ya Abdalla Ahmed mwaka 2009, akiwa na lengo la kujenga hospitali na eneo la jitimai.

Hata hivyo, alisema, alizuiliwa kulitumia eneo hilo baada ya kuelezwa na mamlaka za ardhi kwamba linatakiwa kubakia wazi kwa ajili ya uendelezaji wa uwanja wa ndege.

“Sikupinga kwa vile hayo ni maamuzi ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi wake. Lakini cha kushangaza, eneo hilo likaja kuvamiwa na kugaiwa viwanja bila ya mimi ninayelimiki kujuulishwa, hili halikubaliki,” alieleza Juma.

Alisema, baada ya kulifuatilia hilo kwenye wizara husika ya ardhi, hakupatiwa majibu zaidi ya kuzungushwa na kupewa vitisho kutoka kwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo ya umma.

“Nilihangaikia eneo langu kwa muda mrefu bila ya kujua hatma yake, lakini, sasa naamini haki yangu itarejea,” aliongeza.

Mmoja wa mwanafamilia wanaosimamia eneo hilo, Abdulwahid Abdalla Ahmed, alisema, waliliuza eneo hilo kwa mmiliki wa sasa kwa taratibu zote baada ya kulimiliki kihalali chini ya familia ya marehemu mzazi wao huyo.

Hata hivyo, alisema, alishangaa baada ya kupata taarifa ya uvamizi wa eneo hilo nje ya umiliki wa waliyemuuzia, Said Mbuzi, na kukatwa viwanja.

“Mimi ni umri wa miaka 60 sasa, waraka wa eneo hili huu hapa, sasa vipi lihodhiwe na kukatwa viwanja nje ya mmiliki tunayemtambua kama familia”, alihoji.

Akizungumza na wajumbe wa bodi ya uhaulishaji ardhi hivi karibuni, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe Juma aliitaka bodi hiyo kutokuwa chanzo cha migogoro na badala yake kuwa watatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria zinazowaongoza.

Alisema, kufanya hivyo kutasaidia kuondoa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza siku hadi siku na kupelekea malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali na taasisi zake jambo alilosema linapaswa kumalizika.