NA TATU MAKAME

JESHI la poIisi Zanzibar limeeleza kuwa, hali ilikuwa shwari katika maeneo mengi ya visiwa vya Zanzibar wakati wa kipindi cha sikukuu ya krismass wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa za makamanda wa polisi wa mikoa mbali mbali ya unguja, sikukuu hiyo ilimalizika salama licha ya kuwepo kwa matukio madogomadogo.

Akizungumza na mmoja ya waandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Awadhi Juma Haji, alisema skukuu hiyo ilimalizika kwa amani na utulivu na hakuna tukio lililoripotiwa la kuhujumiwa kwa nyumba za ibada wala raia.

Alifahamisha kuwa utulivu huo umekuja kufuatia jeshi hilo, kuimarisha ulinzi katika maeneo yote yakiwemo ya nyumba za ibada na makaazi ya watu.

Hata hivyo Kamanda Awadhi, aliwataka wananchi kuendelea kuimarisha amani na kwamba polisi wataendelea kutimiza wajibu wao kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mkoa huo katika kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi Haji Abdalla Haji, aliliambia gazeti hili kwamba hali ya amani na utulivu ilitawala ndani ya mkoa katika kipindi hicho kutokana na juhudi zilizofanywa na jeshi lake kuimarisha ulinzi.

Alisema watendaji wa jeshi hilo wakishirikia na vikundi vya ulinzi shirikishi, walifanya kazi kubwa ya kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwemo fukwe za kitalii na nyumba za ibada.

Hata hivyo alieleza kuwa jeshi la polisi litaendelea kufanya doria na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana nalo kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kwa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kukabiliana na uhalifu.

Kuhusu matayarisho ya sikukuu ya mwaka mpya baadae wiki hii, Kamanda Haji aliwataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhsalivu na uvunjifu wa sheria vikiwemo vya kuchora barabara kwani jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kupambana na wahalifu.

Katika mkoa wa Kusini Unguja, Kamanda wa polisi mkoani humo Suleiman Hassan Suleiman, alieleza kuwa hali ilikuwa shwari na kwamba wananchi wanapaswa kuendeleza hali hiyo katika kipindi cha kuuaga mwaka 2020 na kuukaribisha mwaka 2021.

Alieleza kuwa katika kipindi hicho, polisi mkoani humo

Wakiwa katika doria kwenye maeneo mbali mbali ya mkoa huo, Disemba 25, mwaka huu majira ya saa 6:30 walimkamata Ali Faki Ali (34) mkaazi wa Kiponda mjini Unguja na misokoto 15 ya bangi huko Michanvi Kae.

Alisema misokoto hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwenye paketi ya sigara ambapo pia alipatikana na fedha taslim Dola za kimarekani 200 zenye fedha za Tanzania shilingi 3,600 ambapo mtuhumiwa huyo yupo chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

Aidha kamanda suleimani alieleza pia walimtia nguvuni Juma Makame Ussi (29) mkaazi wa Paje akiwa na unga sampuli  ya vidonge 13  vinavyodhaniwa kuwa ni  madawa ya kulevya.

“Tukio hilo limetokea majira ya saa 6:45 mchana huko Bwejuu, Wilaya ya Kusini Unguja, akiwa na vidonge vyeupe vinane, kahawia (Brown) nne na bahari kimoja vilivyokuwa kwenye plastiki vikiwa vimehifadhiwa katika mfuko mweupe laini  na kuingizwa kwenye paketi ya sigara aliyokutwa nayo mikononi,” alifafanua kamanda Suleiman.

Aliongea kuwa katika kupambana na uhalifu, polisi mkoani humo litaendelea kufanya dori ana kuweka ulinzi ambao utawafanya wananchi wa mkoa huo kusheherekea kwa amani sikukuu za mwisho wa mwaka.