NA MARYAM HASSAN

KIJANA wa miaka 21 mkaazi wa sogea, amepelekwa rumande hadi Disemba 31 mwaka huu baada ya kushitakiwa katika mahakama ya mkoa Vuga kwa makosa mawili tofauti, ikiwepo kubaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15.

Kijana huyo ni Idrisa Ame Maisha, amefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira na kusomewa shitaka lake na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mohammed Abdalla.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka kwa mshitakiwa huyo, inadaiwa kuwa alitenda kosa la kurorosha mtoto huyo Julai 3 mwaka huu majira ya saa 10:00 za jioni, huko Sogea wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo, alimtorosha mtoto huyo ambaye hajaolewa na yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake na kumpeleka nyumbani kwa rafiki yake Sogea bila ya ridhaa ya wazazi wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha inadaiwa kuwa baada ya kumtorosha, alitenda kosa la kubaka ambalo ni kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na 109 (1) sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya makosa ya Jinai Zanzibar.

Pia inadaiwa kuwa, Julai 16 mwaka huu majira ya saa 9:30 za mchana huko Magomeni wilaya ya Mijini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alimuingilia tena mtoto huyo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa makosa yote matatu, mshitakiwa huyo alikataa na kuomba kupewa dhamana suala ambalo lilipingwa.

Wakili Shamsi, alisema kosa alilofanya mshitakiwa huyo ni miongoni na mwa makosa ambayo hayana dhamana.

 Hivyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, kwa sababu tayari upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Disemba 31 mwaka huu kwa kuanza kusikilizwa ushahidi na mshitakiwa amepelekwa rumande.