LONDON, England

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amewataka mashabiki wa kikosi hicho kuvuta subira zaidi kwa matarajio kwamba, wachezaji wake  wataanza kufanya vyema hivi karibuni na kuleta matokeo mazuri.

Hata hivyo Arteta ametilia shaka kiwango kwa baadhi ya wachezaji wake wazoefu, hoja ambayo imeungwa mkono na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Alan Shearer, ambaye anahofia kwamba huenda Arsenal watateremshwa daraja mwishoni mwa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu.

Kichapo cha 2-1 ambacho Arsenal walichopewa na Everton wiki iliyopita kilifanya Arsenal ambao sasa wamepoteza mechi nane kati ya 14 zilizopita, kuweka rekodi ya mwanzo mbaya zaidi  ya ligi tangu 1974-75.

Masaibu ya Arteta na Arsenal huenda sasa yakaongezeka zaidi katika kipindi cha wiki moja ijayo. Kichapo kutoka kwa Everton kiliwaning’iniza Arsenal pembamba kiasi kwamba kwa sasa ni alama nne pekee ndizo zinazowadumisha nje ya mduara wa timu tatu za mwisho zinazokodolea macho hatari ya kushushwa daraja.

Kubwa zaidi linalotatiza Arsenal ni utovu wa nidhamu miongoni mwa wachezaji wake  wazoefu na ubutu wa washambuliaji  ambao hawajawahi kufunga bao lolote la kawaida isipokuwa kupitia penalti kutokana na mechi tano zilizopita za EPL ugenini.

Bao lililopachikwa wavuni na Nicolas Pepe dhidi ya Everton lilikuwa lake la pili msimu huu na lilitokana na penalti sawa na la kwanza msimu huu.