LONDON, England
KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amewataka mashabiki wa kikosi hicho kuvuta subira zaidi kwa matarajio kwamba wanasoka wake watajinyanyua hivi karibuni na kuanza kupata matokeo ya kuridhisha.

Ingawa hivyo, Arteta ametilia shaka kiwango cha kujitolea kwa baadhi ya wachezaji wake wazoefu, hoja ambayo imeungwa mkono na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, Alan Shearer, ambaye anahofia kwamba huenda Arsenal watateremshwa daraja mwishoni mwa kampeni za Ligi Kuu ya England msimu huu.

Kichapo cha magoli 2-1 ambacho Arsenal walichopewa na Everton mnamo Disemba 19, kiliwafanya wapoteze mechi nane kati ya 14 zilizopita na kuweka rekodi ya mwanzo mbaya zaidi ligini tangu 1974-75.

Kipigo hicho kiliacha Arsenal katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14 pekee.
Masaibu ya Arteta na Arsenal huenda sasa yakaongezeka zaidi katika kipindi cha wiki moja ijayo ikizingatiwa kwamba walikuwa na kibarua kigumu dhidi ya Manchester City katika robo fainali za Kombe la Carabao na kukubali magoli 4-1 kabla ya kuwaalika Chelsea kwenye EPL.

Arsenal sasa ni pointi nne pekee ndizo zinazowadumisha nje ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho vinavyokodolea macho hatari ya kushushwa ngazi.

Kubwa zaidi linalotatiza Arsenal ni utovu wa nidhamu miongoni mwa wanasoka wazoefu na ubutu wa washambuliaji ambao hawajawahi kufunga bao lolote la kawaida isipokuwa kupitia penalti kutokana na mechi tano zilizopita za EPL ugenini.

Bao lililopachikwa wavuni na Nicolas Pepe dhidi ya Everton lilikuwa lake la pili ligini msimu huu na lilitokana na penalti sawa na la kwanza msimu huu.
Utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukiandama Arsenal katika mechi kadhaa zilizopita bado ulidhihirika dhidi ya Everton baada ya Dani Ceballos aliyeponea kuonyeshwa kadi nyekundu kumchezea visivyo kiungo Yerry Mina.