NA TATU MAKAME

IMEELEZWA kuwa Asasi za kiraia zina wajibu wa kuchangia na kushirikiana na serikali kwenye mikakati ya kukuza uchumi wa taifa kwa kupiga vita vitendo vya ufisadi, rushwa na ubadhirifu.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, wakati akilifungua tamasha la 14 la asasi za kiraia katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Alisema siku zote asasi za kiraia zinakuwa daraja la kuwaunganisha wananchi na serikali yao katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayolenga kuimarisha hali za maisha yao.

Dk. Mwinyi alisema serikali inahitaji kuwa na Zanzibar iliyoungana na kwamba tofauti za kifikra, imani za dini, itikadi za siasa, rangi, ukanda, jinsia zisiwe sababu ya maafa bali jamii ichote kutoka utajiri wa tofauti hizo.

Alisema ASASI zina nafasi kubwa ya kuyabaini mapungufu ya kiutendaji serikalini kupitia utekelezaji wa shughuli zao hivyo zinapaswa kuihudumia na kuendelea kuwa karibu na jamii.

Aidha Dk. Mwinyi alisema anayaelewa mazingira ya wadau wa asasi za kiraia hasa upatikanaji wa fedha ambao kwa kiasi kikubwa unategemea wafadhili kutoka nje ya nchi ambao umekumbwa na changamoto kubwa.

Alisema uhaba wa rasilimali fedha, mifumo ya kisheria iliyopitwa na wakati na masharti yanayokwenda sambamba na ufadhili huo vinafiza kasi na mazingira ya kukua na kushamiri kwa asasi za kiraia kuwa na dhiki.

Alifahamisha kwamba changamoto hizo kwa ujumla zimekuwa zikirejesha nyuma jitihada za asasi hizo za kuungana na serikali katika utoaji wa huduma na hili limethibitika kwa baadhi ya asasi hizo kuanzishwa zikiwa na dira, dhamira na malengo mazuri lakini zinakufa kipindi kifupi baada ya kukosa ufadhili.

Alisema inapendeza kuona hivi sasa zipo asasi za kiraia zipatazo 2,000 katika ngazi mbali mbali zikihitajiwa zote ingawaje katika mazingira ya sasa ni chache mno zinazoonekana au kusikika.

Alibainisha kwamba kwa vile suala la utungaji wa sera na sheria ni wajibu wa serikali na zipo changamoto zinazoihusu serikali moja kwa moja hivyo, alisema kamwe hatopenda kuona vipo vikwazo wakati serikali ikitambua wazi mchango unaotolewa na taasisi hizo.

Aliwaeleza wadau hao wa asasi za kiraia kwamba hivi sasa mchakato wa utengenezaji wa sheria ya jumuiya zisizo za kiserikali Zanzibar unaendelea na jitihada zimezingatiwa katika kupata sheria rafiki zitakazotokana na ushiriki wao katika hatua mbali mbali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza The Foundation for Civil Society kwa kuwa karibu na asasi za kiraia katika kuzisaidia kifedha na kiutaalamu ambazo nyingi hivi sasa zimeweza kukomaa.

Akitoa maelezo katika tamasha hilo, Mjumbe wa Bodi wa ‘The Foundation for Civic Society’, Munira Said Humud, alisema kwa vile asasi za kiraia ni mtetezi wa jamii ipo haja ya kuongezwa kwa ushirikiano na wadau wote ili kuona dhamira hiyo inafanikiwa vyema.

Munira alisema ushirikishwaji wa asasi za kiraia katika maendeleo ya taifa na jamii haina mjadala wakati huu kutokana na malengo yake moja kwa moja yanamgusa mwananchi katika maeneo yake yote ya ustawi.

Naye Mwenyekiti wa Mwamvuli wa Asasi za kiraia Zanzibar (ANGOZA) Asha Aboud Mzee, alisema asasi za kiraia zimekuwa na utamaduni wa kuendeleza matamasha kila mwaka yanayoongeza wigo wa ufanisi katika kuimarisha uchumi na usawi wa jamii yote ya wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Alisema utawala bora na uwajibikaji unaoendelea kusimamiwa na serikali ya awamu ya nane ni ishara njema ya muelekeo wa kushamiri kwa kasi ya uchumi sambamba na kuziba miyanya ya rushwa, ubadhirifu na uzembe.

Mapema akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Tamasha hilo la nane la asasi za kiraia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, alisema serikali inatambua mchango unaotolewa na Asasi za Kiraia katika maendeleo ya taifa.

Masoud alisema ni vyema kwa wadau wa asasi hizo wakaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika muelekeo wa kumkomboa mwananchi zikijitathmini upya malengo yao ili ziende sambamba na dhamira ya dhati ya serikali kuu katika kuwahudumia wananchi.