NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYEDAIWA kumshambulia mwanamke, ametakiwa kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kopi ya kitambulisho na barua ya Sheha.

Hassan Seif Salum (35), alipewa dhamana hiyo baada ya kukataa kosa aliloshitakiwa mahakaamni hapo la shambulio la kuumiza mwili.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana, hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, Suleiman Yussuf, kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la shambulio la kuumiza mwili kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa, alimshambulia Nai William Molel kwa kumpiga kiatu kichwani, ngumi za kichwa, kumgongesha kwenye ukuta na kitanda na kumsababishia kupata maumivu mwilini mwake, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Mei 30 mwaka huu saa 11:00 jioni huko Jang’ombe wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mahahakama ilikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Disemba 30 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.