NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYEDAIWA kuvunja TV flat skirini na meza mbili za kioo zenye makisio ya thamani ya shilingi 1,400,000 amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la Mohammed Abass Rashid (53) mkaazi wa Kwalinato wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo na kusomwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, Soud Said, ilidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuharibu mali ya mtu kwa makusudi, kinyume na kifungu cha 326 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa mbele ya Hakimu Asya Abdalla Ali kuwa, Januari 7 mwaka huu saa 4:00 usiku huko Kikwajuni, bila ya halali na kwa makusudi, alivunja TV flat pamoja na meza mbili za kioo mali ya Amini Mohammed Amini, vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi 1,400,000 kwa kukisia, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Akizungumzia suala la kupatiwa dhamana kwa mshitakiwa huyo, Wakili Soud alisema hana pingamizi ikiwa mshitakiwa huyo atakuwa na wadhamini madhubuti watakaomchukulia dhamana mahakamani hapo.

Hakimu Asya alisema, dhamana ya mshitakiwa huyo ipo wazi ikiwa atajidhamini mwenyewe kwa shilingi 1,000,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini  wawili.

Kwa mujibu wa Hakimu huyo, kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi na kuwasilisha vitambulisho vyao vya Mzanzibari mkaazi na barua za Sheha, zinazoonesha nambari ya nyumba na picha zao.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.