NA KHAMISUU ABDALLAH

AHMADA Iddi Mohammed (30) mkaazi wa Amani, amefikishwa mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kwa kosa la kuweka gari sehemu hatarishi.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo akipatikana na kosa la kuweka gari sehemu hatarishi, kinyume na kifungu cha 143 cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa, akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 478 AB inayokwenda njia namba 510 akitokea upande wa Michenzani kuelekea Mwembekisonge, alipatikana akiwa amesimamisha gari hiyo katikati ya barabara na kupakia abiria  na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Disemba 10 mwaka huu, majira ya saa 11:05 jioni huko Kisiwandui Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mkini Magharibi Unguja.

Aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe kwa madai kuwa ndio kosa lake la mwanzo, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.

 Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 20,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja, ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaodharau sheria za njia.

Mshitakiwa huyo akifanikiwa kulipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo kama alivyotakiwa na Hakimu Nassem.