Ayoub aahidi vitambulisho wajasiriamali

NA MWANAJUMA MMANGA

MKUU wa mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub amesema serikali   ina mpango wa kuanzisha vitambulisho maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo ili kuondoa tatizo la mrundikano wa kodi.

Alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara maalumu katika soko la Kinyasini kwa lengo la kusikiliza kero kwa wafanyabiashara wa soko hilo ili kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema serikali imeamua kuanzisha mpango huo ili kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitozwa kodi bila ya mpangilio mzuri hali ambayo inasababisha kushindwa kufikia malengo.

Adha Mkuu huyo wa mkoa, alitoa siku saba kwa uongozi wa Baraza la Mji wilaya ya Kaskazini ‘A’ kuhakikisha anajenga vyoo katika soko hilo ili kutimiza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Wakizungumza baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo wamempongeza Mkuu huyo wa mkoa kwa uamuzi wake wa kusikiliza kero za wafanyabiashara na kumuomba kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Hata hivyo walieleza baadhi ya changamoto zao ikiwemo tatizo la mrundikano wa kodi, ukosefu wa vyoo, pamoja na kuishauri serikali kujenga ukuta katika eneo la mbele ya soko hilo ili kuweka ulinzi wa uhakika wa bidhaa zao.