NA MWANDISHI WETU
KIKOSI cha Azam FC juzi usiku Disemba 26 kimetinga hatua ya nne kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya tatu dhidi ya Magereza FC.


Azam FC imeshinda kwa jumla ya mabao 2-0 na kuwafanya wakamilishe dakika 90 wakiwa washindi huku mlinda mlango wao Wilbol Maseke akilinda lango lake bila kufungwa.


Mashabiki wa klabu ya Azam FC walishuhudia mabao hayo yakipachikwa na Obrey Chirwa dakika ya 24 na Never Tigere dakika ya 65.


Azam iliugawa mchezo kwa vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza Chirwa alipachika bao hilo kwa kichwa akitumia kona ya Never Tigere.


Kipindi cha pili Azam ilipata bao kupitia kwa Tigere ambaye amekuwa nyota wa mchezo akihusika kwenye mabao yote mawili, akifunga bao la pili na kutoa pasi moja ya bao.


Taji la Kombe la Shirikisho kwa sasa lipo mikononi mwa klabu ya Simba ambao jana usiku walianza kutetea kikombe hicho mbele ya Majimaji ya Songea, Uwanja wa Mkapa.