NA HUSNA MOHAMMED

NI hapo majuzi tu Zanzibar ilikuwa mwenyeji wa kongamano la Kiswahili la Kimataifa ambapo wageni kadhaa kutoka nchi mbalimbali walihudhuria kwa lengo la kukumbushana kuhusiana na mukhtadha mzima wa lugha hiyo.

Kama inavyoeleweka kuwa Zanzibar ni kitovu cha lugha fasaha ya Kiswahili katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati na dunia kwa ujumla.

Si Zanzibar tu, lakini Kiswahili ni lugha ya taifa kiasi kwamba watanzania wanajivunia kuwa na lugha moja licha ya makabila na lahaja kibao zilizopo.

Kwa kuwa Zanzibar ndio penye Kiswahili fasaha, watu wengi hufika kujifunza Kiswahili huku wakijua fika kuwa Kiswahili fasaha hupatikana hapa.

Iloiyokuwa taasisi ya Kiswahili na lugha za Kigeni (TAKILUKI) sasa SUZA ndio wageni wengi walifika kujifunza lugha hiyo na baadae kwenda nchini kwao nao kuwafunza watu wengine.

Katika miaka ya hivi karibuni lugha ya Kiswahili imekuwa ikiharibiwa kwa kuingiza misamiati ambayo inaendana nje kabisa na utamaduni wa Kiswahili fasaha.

Ili kuifanya lugha ya Kiswahili izidi kumea, lazima iwe na misamiati ya kutosha  katika Nyanja ya kiufundi, teknolojia ya Habari na mawasiliano, sanaa, sheria, michezo,dini na Nyanja zote za kiuchumi kwa lengo la kuwa na nguvu kubwa itakayojitosheleza ili kuepuka kuwa fukara kwa kutegemea misamiati ya Lugha nyengine.

Kinachoonekana sasa ni kuweko Utamaduni wa kukivuruga Kiswahili bila ya aibu hasa kwa Wanajamii walio wengi ambao hufuata mkumbo jambo ambalo huleta athari isiyopendeza katika matamshi ya Lugha yenyewe inayo lahaja za kupendeza katika uzungumzaji wake.

Ili Kiswahili hicho kiweze kudumu Wanahabari na Wasomi ndio wanaotegemewa katika kuiendeleza Lugha hiyo kwa kuwa makini katika matumizi yake hasa wakati wanapotoa Taarifa mbali mbali kwa wana Jamii.

Mbali na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} kwa kushirikiana na Taasisi tofauti za Serikali na hata za kiraia ni lazima Kiswahili kitiliwe mkazo kutumika katika shughuli za kimataifa kama ilivyo sasa.

Ni wazi kuwa juhudi zimekifanya Kiswahili kuwa Lugha ya Saba kati ya Lugha zenye kuzungunzwa na Mataifa mbali mbali kukiwa na idadi ya wanaozungumza na kukifahamu inayokisiwa kufikia Watu takriban Milioni 160 Idadi inayoongezeka kwa haraka kadri ya miaka inavyosonga mbele.

Tafsiri ya Takwimu hizo ni kwamba juhudi hizo za pamoja za kukikuza na kukitangaza Kiswahili zinaendelea kutoa matunda mazuri hasa kwa vile tayari kimesharidhiwa kuwa Lugha inayozungumzwa ndani ya Mikutano ya Viongozi wa Umoja wa Afrika {AU} na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika {SADC}.

Hata hivyo, hakuna budi kutanabahisha kwamba Historia inafunza kuwa ili Lugha yoyote iendelee kuwepo, ikue, isambae na iwe inatumika katika Nyanja tofauti, lazima iwepo mipango na jitihada maalum za kufikia huko  kwa vile ni chombo cha  mawasiliano miongoni mwa Wanaadamu.

Ili kutambua umuhimu wa Lugha ya Kiswahili jitihada kubwa bado zinahitajika kukiendeleza na kuitunza Lugha ya Kiswahili huku Utafiti kwenye maeneo ya Fasihi na Isimu pamoja na Tamaduni za Asili zikiendelezwa.

 Ujumbe wa Kongamano hilo la Mwaka huu unaoeleza “Tuchangamkieni Fursa za Soko la Kiswahili Duniani”, ambapo kwa Zanzibar zinaonekana kumezwa na Tanzania bara na Kenya huku wazanzibari ambao ni weledi wa lugha hiyo wakipoteza fursa hizo za ajira.

Imefika wakati baraza la Kiswahili Zanzibar likafanya tathmini ya kutosha ili kuona kwamba Zanzibar inafaidika vipi katika soko hilo la ajira? Sambamba na kutafuta mbinu madhubuti ili kuona inafaidika katika fursa hizo.