NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Black Sailor imeibuka kidedea mbele ya Mlandege baada ya kutoka na ushindi wa bao 1-0, katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar uliochezwa jana.

Mchezo huo uliokuwa ukitumbuizwa na ngoma ya mdundiko kutoka kwa mashabiki wa Mlandege ulichezwa majira ya saa 10: 00 za jioni uwanjani hapo.

Ushindi wa timu hiyo unawafanya wafikishe pointi 11 na kupanda hadi nafasi ya tano kutoka wa 10 katika msimamo wa ligi hiyo ambayo inaongozwa na KMKM wenye pointi 16.

Katika mchezo huo Black Sailor walipata bao mnamo dakika ya nane lililofungwa na Yussuf Idrissa Iddi.

Miamba hiyo ambayo ligi hiyo wameianza kwa kusuasua ilicheza kwa kushambuliana na Mlandege ikijaribu kujenga mashambulizi ya kushtukiza kwa lengo la kutaka kusawazisha bao hilo, lakini walishindwa kusawazisha.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kupigwa michezo miwili ambapo katika uwanja wa Amaan KVZ itacheza na KMKM na Polisi na JKU watacheza uwanja wa Mao Zedong A.