NA MWANAJUMA MMANGA

BARAZA la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), limesema serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za chama cha Judo (ZJA), ili kuhakikisha  mchezo huo unaendelea na kuleta maendeleo.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Suleiman Pandu Kweleza, wakati akizindua mashindano ya 2020 ya mchezo wa judo huko ukumbi wa Judo Amani.

Alisema lengo la serikali ni kuimarisha mchezo wa judo pamoja na michezo mingine.

Alisema  kuna changamoto nyingi zinazozikabili klabu ikiwa ni pamoja na suala zima la maeneo ya kufanyia shughuli zao, ambazo kama serikali imekuwa ikikabiliana nazo ili waweze kufikia malengo yao.

Alisema hivi karibuni wamefanya ukaguzi wa jengo la judo kwa upande wa Pemba ambalo   pia limetokana na mchango mkubwa uliotolewa na chama hicho.

Kweleza alitumia fursa hiyo kumpongeza rais wa chama hicho Tsuyoshi Shimaoka kwa mchango mkubwa alioutoa katika kusaidia upatikanaji wa kiwanja cha judo kisiwani Pemba na kumuomba rais huyo kuendelea kusaidia ujenzi wa jengo hilo na mengine ili kuona mchezo huo unaimarika na kukua zaidi.

Nae rais wa Judo Zanzibar Tsuyoshi Shimaoka alisema mashindano hayo ya 18 kwa Zanzibar yalishirikisha wachezaji wa uzito tofauti kutoka klabu mbali mbali za  Tanzania bara na Zanzibar.

Alisema wanatarajia mashindano hayo yatachagua wachezaji wa wazuri kwa kila uzito kwa ajili ya kushiriki mashindano mbali mbali ya mchezo huo yakiwemo ya Afrika Mashariki na kati, klabu bingwa na mashindano ya Dunia ya  Olimpiki yatakayofanyika mwakani nchini  Japan.

Aidha aliishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo  na serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini na wadau mbali mbali kama vile Zanzibar Sport and Culture Support Oganization na marafiki wa Japan kwa kushirikiana nao kwa hali na mali wakati wa mashindano kama hayo na kitaifa na kimataifa .

Jumla ya timu sita zilishiriki mashindano hayo kutoka Tanzania  bara na visiwani.

Timu hizo ni Mageneza,  Kisutu na Polisi kwa Tanzania Bara  na kwa upande wa Zanzibar Kibodokan, Pemba Kengeja, Pemba Budokan, ambazo wachezaji wake walishiriki kwa uzito kuanzia kilo 60,66,73 81 na 90.