KATHMANDU,NEPAL

NEPAL inatarajiwa kufanya uchaguzi mwakani baada bunge kuvunjwa ghafla.

Hatua hiyo ilichochewa na mivutano kati ya waziri mkuu na wanachama wa chama chake.

Serikali ya Waziri Mkuu K.P. Sharma Oli imekuwa ikishutumiwa kwa madai ya rushwa na kushindwa kushughulikia janga la virusi vya corona ipasavyo.

Lakini uamuzi wake wa kuitisha uchaguzi mpya unatokana na mivutano ya miezi kadhaa na Pushpa Kamal Dahal, kiongozi wa zamani wa waasi ambaye alimsaidia Oli kuingia madarakani wakati vyama vyao vya kisiasa vilipoungana mnamo mwaka 2018.

Wawili hao hapo awali walikuwa wanazozana juu ya makubaliano yao ya kugawana madaraka na ukosefu wa mashauriano.

Uchaguzi mpya utafanyika miezi ya Aprili na Mei mwakani, ilisema ofisi ya Rais Bidhya Devi Bhandari katika taarifa baada ya kukubali kuvunjwa kwa bunge.