NA KHAMISUU ABDALLAH

Wanachama wa CCM wameanza kujipanga kushinda katika uchaguzi mdogo utaofanyika katika Jimbo la Pandani Kisiwani Pemba na Wadi Kinuni kwa nafasi ya Udiwani utaofanyika Machi 28, mwaka 202.

Kufanyika kwa uchaguzi katika maeneo hayo kunatokana na aliyekuwa Mwakilishi mteule wa Jimbo hilo Abubakar Khamis Bakar, na Diwani wa wadi ya Kinuni Suleiman Hassan Mohammed kufariki dunia.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) hivi karibuni imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Pandani kisiwani Pemba na Kinuni kwa nafasi ya udiwani ifikapo Machi 28 mwaka 2021.

Wanachama hao wameeeleza wameanza kujipanga, ili kuona Chama cha Mapinduzi kinashinda katika uchaguzi huo, kwa vile wanakila sababu ya kushinda katika uchaguzi huo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mbunge wa viti Maalum, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Saada Mansour alisema, Chama cha Mapinduzi tayari kimeshajipanga kwa kusimamisha mgombea ambaye atashinda katika uchaguzi huo, ili kuendeleza rikodi yake ya ushindi ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania.

Alisema Jumuiya yao ya UWT Mkoa wa Kaskazini ipo tayari kuona inashirikiana na Mikoa mingine  itayofanyika uchaguzi huo, ili kuhakikisha wanawake wanajitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo.

Mapema wiki iliyopita Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Mabrouk Jabu Makame, alisema Machi 3, hadi 11, mwaka huo itakuwa ni uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi.

Aidha alisema Machi 12 mwaka huo itakuwa ni uteuzi wa wagombea, Machi 13 hadi 26 ni kampeni za uchaguzi na Machi 28 ni siku ya upigaji wa kura katika jimbo hilo na wadi.

Makamo huyo alibanisha kwamba ZEC imefanya hivyo kwa kuzingatia maelekezo ya sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.

Alisema, tume inawajibika kufanya uchaguzi huo chini ya kifungu cha 40 (2) na (3) cha sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kuendesha uchaguzi mdogo kwa nafasi hizo si chini ya miezi minne na isizidi miezi 12 baada ya kutokea tukio lilopelekea uchaguzi mdogo kufanyika.

Aidha, alibainisha kuwa sheria hiyo ilieleza kuwa ni jukumu la tume hiyo kuendesha na kusimamia uchaguzi mkuu na kuendesha uchaguzi mdogo pale inapotokea sababu ya kufanyika kwa uchaguzi baada ya kupata taarifa kutoka kwa mamlaka husika.

Alisema ZEC, ilipokea taarifa za kuwepo kwa nafasi za wazi kwa viongozi wateule ambao wamefariki dunia.