NA HAFSA GOLO

CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja, kimesema kinatarajia kuandika historia mpya ndani ya mkoa huo ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii katika serikali ya awamu ya nane.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mula Othman Zubeir, wakati akizungumza na gazeti hili ofisi ya Mkoa wa Chama hicho Mahonda.

Alisema wanaCCM na wananchi wa mkoa huo wanamategemeo mazuri kwa serikali hiyo kupata fursa mbali mbali za ajira ambazo zitakuwa ni sehemu ya kuleta mabadiliko kwao ya maendeleo.

Katibu alisema miongoni mwa mambo wanayoyatarajia yanaweza kuwa ni chachu ya kutimiza ndoto zao ni pamoja na serikali kuweka nia na mpango wa kuwekeza miradi ya kiuchumi katika mkoa huo ikiwemo ujenzi wa bandari mbili ya kuteremshia mafuta na gesi na meli ya kitalii.

Alisema eneo hilo limewagusa vijana,wanawake na hata wazee hivyo wamekuwa wakijiandaa kitaaluma na kifkra juu ya matumizi ya ajira mbadala zitakazoweza kujitokeza katika eneo hilo ili waweze kujiajiri.

Mbali na hilo, Katibu huyo alisema jambo jengine ambalo kwa sasa limeleta gumzo na matumaini kwa wakaazi wa mkoa huo ni pamoja na kauli  njema za Dk.Mwinyi wakati wa akinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi,ahadi na utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi hasa suala la changamoto ya ajira.

“Kaskazini kuna ukanda wa mahoteli na Bangaloo zisizopungua 1200 hivyo ahadi ya Dk.Mwinyi ya kusimamia  ajira isiyo na taaluma yoyote kwa wazawa litasaidia kutoa fursa nyengine kwa vijana “,alisema.

Alisema halkadhalika suala la usimamizi wa serikali ya awamu ya nane juu ya miradi inayoekezwa vijiji kuhakikisha inakuwa ni sehemu ya kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo sehemu husika ikiwemo maji safi na salama, elimu na vituo vya afya nalo limepokelewa vyema kwa wananchi wa mkao huo na hatimae kutarajia makubwa zaidi.

Hata hivyo, katibu huyo alisema wakati wananchi hao wakijiandaa kutumia fursa hizo na  neema zilizoahidiwa na Rais Mwinyi , ni vyema kuendelea kudumisha amani na utulivu sambamba na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wao wa jimbo.

 Alitumia fursa hiyo, kuwakumbusha wabunge, wawakilishi na madiwani  wa mkoa huo kufanyakazi kwa pamoja kwani ndio njia pekee itakayosaidia utekelezaji wa ilani kwa kasi na muda unaostahiki.

“Tayari nimeshakaa na viongozi wangu wote wa CCM mkoani humo kuwafahamisha umuhimu wa kuchapakazi kwa timu na kuondokana na tofauti “,alisema.

Alisema katika kikao hicho alitaka kila kiongozi wa jimbo kuandaa mpango kazi wa miaka mitano wakijumuisha ahadi walizoziweka ili Chama Mkoa kisimamie mpango huo kwa kila jimbo.

Mapema gazeti hili lilifanya mahojiano na wananchi mbali mbali wa mkoa huo ambapo walisema wanatarajia katika serikali ya awamu ya nane neema ya maendeleo sambamba na kuimarika kwa utawala bora unaozingatia haki na wajibu kwao.

Mmoja wa wananchi hao mkaazi wa Mahonda, Patima Ali alisema, anaamini kwamba kutakuwa na kasi ya kiuchumi na kijamii hasa ikizingatiwa serikali ya awamu ya nane imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha viongozi na wananchi wanatimiza wajibu wao wa kuchapakazi.

“ Zanzibar ni nchi ya kisiwa na kikawaida nchi nyingi kama hizi duniani zimekuwa na fursa nyingi za kibiashara changamoto iliyokuwepo ni wananchi kutojikubalisha kutii na kufuata maelekezo ya viongozi lakini serikali hii haina mzaha tutafika tu”,alisema.

Nae Ali Juma Ali, Mkwajuni  alisema ili kufikia azma na mipango ya maendeleo ni muhimu kila mmja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake bila ya kushurutizwa.