CHINA na Umoja wa Ulaya, EU zimehitimisha majadiliano yaliyochukua miaka saba ya makubaliano ya uwekezaji wa biashara baina ya pande hizo.

Viongozi wa China na EU walifanya mkutano kwa njia ya video na kuafikiana juu ya makubaliano hayo yaliyolenga kukuza uwekezaji baina ya pande hizo mbili.

Angalizo la majadiliano ya pande hizo, lilikuwa kuwalinda wafanyakazi wa China. EU inasema watu kwenye eneo linalojitawala la Xinjiang Uygur wanalazimishwa kufanya kazi na inaitaka China kuboresha hali hiyo.

Suala jengine lililoangaziwa ni hatua zinazochukuliwa nchini China ambapo makampuni ya Ulaya yanalazimishwa kuhamisha teknolojia zao kwa mabadilishano ya kuweza kuingia kwenye soko la nchini humo.

EU imesema China imekubali kutafuta maridhiano ya mkataba wa kimataifa unaopiga marufuku ufanyaji kazi kwa kulazimishwa na kufanya maboresho kwenye suala la uhamishaji wa lazima wa teknolojia.

EU imesema makubaliano hayo ni jitihada kubwa ambazo China haikuwahi kufanya hapo kabla na taifa lingine. Lakini baadhi ya nchi za EU zinasema dhamira ya China juu ya kulindwa kwa wafanyakazi haitoshelezi.