HONG KONG, CHINA

MAHAKAMA moja nchini China imewahukumu hadi miaka mitatu gerezani raia wa Hong Kong waliokamatwa na walinzi wa pwani wa China wakijaribu kukimbilia kisiwa cha Taiwan.

Wanaharakati 12 wanaounga mkono demokrasia na wanafunzi walikamatwa na walinzi wa pwani wa China mwezi Agosti mwaka jana wakijaribu kuingia Taiwan kwa boti.

Wengi wa wanaharakati hao 12 walikuwa wamepewa dhamana wakati wa jaribio la kutoroka baada ya kukamatwa na kushtakiwa kuhusiana na maandamano ya kupinga serikali katika eneo la Hong Kong.

Mmoja wao ni mwanamume aliyekamatwa kwa tuhuma za kukiuka sheria ya usalama wa kitaifa ya eneo hilo.

Hapo juzi mahakama moja katika mji wa kusini mwa China wa Shenzen unaopakana na Hong Kong, ilimhukumu mwanamume na mwanamke kifungo cha miaka mitatu na miaka miwili mtawalia gerezani kwa kuratibu uhamiaji huo kinyume cha sheria. Wanane kati ya hao 12 walihukumiwa kifungo cha miezi saba gerezani.

Waendesha mashitaka wa China waliamua kutowashitaki vijana wawili waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18 walipokamatwa. Wawili hao walikabidhiwa polisi wa Hong Kong ili kudadisiwa.

Mahakama ilisema washukiwa wote 12 walikiri mashitaka, lakini haijatoa maelezo ya kina ya kesi hiyo.