NA HAFSA GOLO

MWENYEKITI wa Chama  Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib, amewataka viongozi wa majimbo kuongeza kasi ya utekelezaji wa ahadi, utatuzi wa kero za wananchi sambamba na ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025, ili kuimarisha imani kwa wapiga kura na wananchi.

Alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na wanaCCM na wananchi wa jimbo la Chumbuni kuhusiana na utekelezaji wa ahadi za viongozi wa jimbo hilo huko Masumbani.

Talib alisema utendaji  kazi wa kasi kwa viongozi hao utaongeza ari na kujenga historia mpya ndani ya CCM kama ilivyokuwa dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ya kuwatatulia kero mbali mbali wananchi na kupata maendeleo.

Alisema wananchi wanahitaji mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo, hivyo iwapo viongozi hao watawajibika vyema matumaini ya wanachi watayafikia .

Aidha Talib alihimiza umuhimu kwa viongozi wa jimbo kuchapakazi kwa mashirikiano sambamba na kusikiliza mahitaji ya miradi ya maendeleo yanayohitajika katika shehia husika, kwani hiyo ndio njia moja wapo itakayotoa fursa ya ushiriki wa wananchi ipasavyo.

Katika hatua nyengine alipongeza juhudi zilizochukuliwa na viongozi wa jimbo la Chumbuni za kusimamia fikra na malengo ya Mzee Abeid Amani Karume ya kujenga viwanda vingi jimboni humo.

“Kitendo cha viongozi wa jimbo la Chumbuni kubuni masuala ya ushoni kwa wananchi wenu kwa kuwapatia vyarahani na huku mkiwa na dhamira ya kuanzisha viwanda vya ushoni mmeonesha nia ya muasisi wetu”,alisema.

Alisema hatua hiyo nayo ipo sambamba na malengo ya serikali ya awamu ya nane kwa kupanua fursa za ajira nchini ili wananchi waweze kujikwamua na umasikini.

Akisimulia historia ya nyuma alisema awamu ya kwanza ya serikali ilijenga zaidi ya viwanda 10 ndani ya jimbo hilo kikiwemo kiwanda cha viatu, sukari, sabuni na kiwanda cha kukarabati magari kilichopo eneo la Karakana.

Nae Katibu wa CCM jimbo la Chumbuni, Mussa Muhamed, alisema atahakikisha anawasimamia kwa karibu viongozi wa jimbo hilo, ili kuona ahadi na matumaini ya wananchi yanaweza kufikiwa katika kipindi kifupi kijacho.

Alisema ufanisi na uwajibikaji uliomakini atahakikisha unachukua nafasi jimboni humo sambamba na kuwajengea uwezo vijana waweze kujiajiri wenyewe bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.

Nae Mbunge wa jimbo la Chumbuni Ussi Salum Pondeza aliahidi kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo wanazitatua kwa wakati kwa kushirikiana na viongozi wengine wa jimbo hilo.

Aliwasisitiza wananchi kushirikiana pamoja viongozi wao wa jimbo ili kuleta mabadiliko ya haraka  ya kimaendeleo katika jimbo lao.