NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya Chuoni jana imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zimamoto katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar uliochezwa uwanja wa Amaan.


Mchezo huo ambao ni wa pili kwa timu hiyo kushinda umewafanya wafikishe pointi saba lakini bado wakiwa wanashikilia nafasi yao ya pili kutoka mkiani.


Katika mchezo huo Chuoni mabao yao yalifungwa na Mundhir Abdalla dakika ya 24 na Khalid Habib dakika ya 87, wakati Zimamoto bao lao lilifungwa na Haruna Abdalla dakika ya 23.


Aidha katika uwanja wa Mao Zedong JKU na KVZ zililazimika kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali.


Miamba hiyo ambayo mara zote wanapokutana wanakuwa na ushindani mkali walienda mapumziko wakiwa hawajafungana.


Katika mchezo huo JKU ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa mchezaji wake Mustafa Hamad Simai dakika ya 62 na kusawazishiwa dakika ya 85 na Mohammed Abdalla Ajib.


Katika uwanja wa Gombani Pemba nako kulikuwa na mchezo kati ya Hard Rock na Mafunzo ambao ulimalizika kwa Mafunzo kushinda mabao 2-1.


Kwa ushindi huo Mafunzo imefikisha pointi 12 nakushika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na KMKM wenye pointi 13.


Ligi hiyo leo itakuwa mapumziko na inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa kupigwa michezo miwili, ambapo uwanja wa Amaan Polisi itacheza na Kipanga na katika uwanja wa Mao Zedong KMKM itacheza na Malindi.