NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya Dula Boy’s bado wameendelea kuandamwa na vichapo katika ligi daraja la Kwanza Kanda ya Unguja baada ya juzi kufungwa na Kilimani City mabao 2-0.


Kichapo hicho ni cha pili mfululizo ambapo mechi iliyopita walifungwa na Ngome mabao 2-1 mchezo uliochezwa uwanja wa Amaan.


Katika mchezo huo wa juzi Dula Boy’s ambao walikuwa wageni licha ya kujaribu kupapatua, lakini walijikuta wakitandikwa mabao hayo ambayo yamezidi kuwaweka katika msongo mkubwa wa mawazo wa kutafuta muarubaini wa kukabiliana nao.


Kilimani City ambao mechi yao ya awali walifungwa mabao 2-1 na New King, katika mchezo huo walicheza kufa na kupona ili kuhakikisha wanaondoka na ushindi.


Mabao yote hayo ya Kilimani City yalifanikiwa kuwekwa kimiyani na mchezaji wao Bakari Mwalimu katika dakika ya tatu na 60.


Aidha katika uwanja wa Kinyasini timu ya New King ikashindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kukubali kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Jang’ombe Boy’s.


Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa kuchezwa mechi tatu, ambapo katika uwanja wa Amaan Jang’ombe Boy’s itashuka kuumana na Taifa ya Jang’ombe , wakati katika uwanja wa Mao Zedong ngome itakipiga na Idumu na huko Jambiani Dula Boy’s itaikaribisha New King.


Michezo mengine Uhamiaji imekubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mchangani FC.
Mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong na kuwa na ushindani wa hali ya juu, uliopelekea kwenda mapumziko wakiwa hawajafungana.


Katika mchezo huo Uhamiaji ambao mechi iliyopita walishinda mabao 2-1 dhidi ya Mchangani United ilijitahidi kucheza ili kutoka na ushindi lakini mwisho wa mchezo ilijikuta ikipata kichapo hicho.
Mchangani FC ambayo mastakimu yake ipo Mchangani bao lao hilo la pekee liliwekwa kimiyani na mchezaji wake Talib Ali dakika ya 54.


Aidha katika uwanja wa Amaan kulikuwa na mchezo wa ligi hiyo uliowakutanisha Mchangani United na Gulioni ambao ulimalizika kwa sare ya kutokufungana.


Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezo mitatu ambapo katika uwanja wa Amaan Taifa Jang’ombe na Jang’ombe Boys watacheza, Dulla boys itakutana na New King nyumbani kwao Jambiani na katika uwanja wa Mao Zedong Ngome itacheza na Idumu.