NA MWANAJUMA MMANGA
MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Rajab Ali Rajab, amemuagiza sheha wa shehia ya Kiombamvua kuwasilisha majina ya wananchi waliopokea fedha zaidi ya shilingi Milioni 25 kutoka kampuni ya Sea Rock Resort Limited zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano na wananchi wa shehia hiyo.
Alisema kwa mujibu wa maelezo aliyoyapata kutoka kwa wananchi, fedha hizo zilipokelewa na kamati ambayo haikuwepo wakati wa kuingia makubaliano na kampuni hiyo kwani kamati halali ilizikataa fedha hizo baada ya kugundua kuwa haziendani na makubaliano ya awali.
Mkuu huyo aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na uongozi wa kampuni hiyo huko Nanjale, shehia ya Kiombamvua kwa lengo la kusikiliza mgogoro uliopo kati ya muwekezaji na wananchi.
Rajab, alisema ni vyema wananchi wakaacha kujihusisha na tabia ya kupokea fedha ambazo haziwahusu ili kuondoa migogoro baina yao na wawekezaji.
Hata hivyo Rajab aliitaka kampuni hiyo kulipa stahiki za wafanyakazi ambao wameitumikia kwa muda mrefu bila ya kulipwa stahiki zao na kuitaka kampuni hiyo kufanya uhakiki wa wafanyakazi wazawa sambamba na kuangalia utekelezaji wa sheria ya utumishi kwa sekta binafsi.
Mapema wakiwasilisha malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa wilaya huyo, wananchi wa Nanjale walisema wamelitumia eneo hilo kwa kipindi cha miaka sita wakifanya shughuli za uvuvi ndipo alipojitokeza muwekezaji huyo aliyedai kuwa amelinunua kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli ya kitalii.
Walisema waliingia mkataba na kampuni hiyo kwa makubaliano ya kupewa gari ya kusafirishia dagaa kutoka ufukweni mwa bahari hadi katika eneo walilokubaliana, ajira kwa wananchi, soko la mazao na ujenzi wa skuli mbili za maandalizi makubaliano ambayo hayajatekelezwa.
Akitoa ufafanuzi Afisa Rasilimali Watu kutoka kampuni ya Sea Rock Resort Limited, Bariki Shayo, alisema kampuni imeshatekeleza baadhi ya makubaliano ikiwemo kukabidhi gari kwa kamati, ujenzi wa skuli moja ya maandalizi katika shehia ya Kiombamvua na kuahidi kulipa stahiki zote kwa wafanyakazi waliosimamishwa kazi.
Hata hivyo aliwaomba wananchi hao kutekeleza makubaliano yao kwa kuacha kutumia eneo la ufukwe kwani kuendelea kutumia eneo hilo kunapunguza uingiaji wa wageni katika Hotel hiyo kutokana na kuchafua mandhari ya eneo hilo.
Baada ya mazungumzo kati ya pande mbili hizo, wananchi hao na mwekezaji walifunga mkataba mwengine utakaoanza utekelezaji wake Disemba 3 mwaka huu, huku serikali ya wilaya ya Kaskazini ‘B’ ikiendelea kufuatilia maswala mengine yanayohusu mgogoro huo.