NA MARYAM HASSAN

DEREVA Mohammed Saleh Mohammed (52) mkaazi wa Mwembe Makumbi, amenusirika kwenda rumande baada ya kusaini bondi ya shilingi 100,000.

Masharti hayo amepewa na Hakimu wa mahakama ya wilaya Mwera, Taki Abdallah Habibu, baada ya mshitakiwa huyo kuomba kupewa dhamana kwa kosa aliloshitakiwa nalo mahakamani hapo.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa kuendesha gari barabarani bila ya hadhari na uangalifu, ambapo mbali na kusaini kima hicho, pia ametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini kima hicho hicho cha fedha.

Pia wadhamini hao wametakiwa kuwasilisha kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi pamoja na barua ya Sheha wa Shehiya wanazoishi.

Akiwa mahakamani hapo, kesi yake ilisomwa na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh.

Wakili huyo alidai kuwa, mshitakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 19 mwaka huu majira ya saa 5:30 usiku huko Kibele wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa akiwa dereva wa gari yenye nambari za usajili SMZ 268 D, aliigonga kwa nyuma gari yenye nambari za usajili Z 268 AX iliiyokuwa ikiendeshwa na Khamis Suleima Khamis na kusababisha uharibifu wa gari zote mbili.

Wakili huyo alisema, kwa kuwa mshitakiwa amekataa kosa lake, aliomba kesi hiyo iahirishwe na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi. Pia ameeleza kuwa, upelelezi wa shauri hilo umekamilika, kwa hatua hiyo mshitakiwa ametimiza masharti aliyopewa na yupo nje kwa dhamana hadi Januari 11 mwaka 2021 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.