NA BENNY MWAIPAJA, DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Isdor Mpango, ametoa muda wa siku tisa kwa Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma  kujieleza kwa maandishi sababu zilizozifanya taasisi zao kuchangia mfuko mkuu wa Serikali chini ya kiwango.

Pia Waziri Mpango ametoa muda huo kwa wakuu hao kwa  kutochangia huduma za jamii pamoja na kutozingatia ukomo wa matumizi ya asilimia 60 ya mapato ghafi ya taasisi na mashirika yao kwa mujibu wa Sheria.

Dk. Mpango ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipokutana na Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma 236 kutoka nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kikazi na taasisi mbalimbali za Serikali, ili kutoa mwelekeo mpya wa utendaji wa taasisi hizo hususan kuimarisha na kuongeza mapato ya Serikali.

“Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali bado hauridhishi. Kwa mwaka 2019/20, mchango wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika pato la Taifa ulikua chini ya asilimia moja (1%), kiwango hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika haya” Alisema Dk. Mpango

Alimwagiza Msajili wa Hazina,  Athumani Mbuttuka, kuhakikisha taarifa hiyo ya maandishi kutoka kwa wakuu hao wa Taasisi inamfikia tarehe 31 Desemba 2020, na kutangaza kufuta likizo za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa Viongozi hao, ili watekeleze maelekezo yake.

Alifafanua kuwa Kifungu cha 47 cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na kifungu cha 8 cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 iliyorekebishwa mwaka 2015, kinazitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo  alisema,  bado kuna Taasisi ambazo zinachangia chini ya kiwango kilichowekwa kisheria na zipo Taasisi na Mashirika hata mchango kwa jamii (CSR) hawatoi kabisa!

Dk. Mpango alisema, kuwa Kifungu cha 46 (1) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na Kifungu cha 10A cha Sheria ya Msajili wa Hazina, iliyorekebishwa mwaka 2015, kinaweka ukomo wa gharama za uendeshaji kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yasiyo ya kibiashara kutozidi asilimia 60 ya mapato ya ghafi lakini bado kuna Taasisi na Mashirika ya Umma zinavunja sheria hiyo.

“Kifungu 46 (2) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 kinaelekeza Taasisi na Mashirika ya Umma kuwasilisha asilimia sabini (70) ya ziada kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuondoa gharama za mishahara na kuzingatia ukomo wa matumizi ya uendeshaji uliotajwa kwenye aya 2.1(b) lakini yapo mashirika na Taasisi hayatekelezi matakwa haya” alisisitiza Dk. Mpango

Aliwaagiza wakuu hao wa Taasisi kuhakikisha kuwa wanapunguza matumizi yasiyo na tija, na yasiyo ya lazima ikiwemo misafara mikubwa ya watendaji na wajumbe wa bodi kutembelea miradi, ili kuziwezesha taasisi zao kuwa na fedha za kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya kijamii na ya kimkakati inayotekelezwa nchini.

“Serikali chini ya uongozi shupavu wa Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa umeme (MW 2115) Mto Rufiji, uboreshaji wa usafiri wa anga na majini, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, Elimu bila ada, usambazaji wa umeme vijiji vyote nchini, na uboreshaji wa huduma za afya na maji” Alifafanua Dk. Mpango.

Alisema Idara zote zinazokusanya maduhuli, na Halmashauri zote lazima zifanye jitihada kubwa zaidi kuongeza ukusanyaji wa  mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, ili kuwezesha kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha za ndani kwa kiwango kikubwa na kwamba mambo hayo yatafanikiwa endapo watendaji hao wataacha kufanyakazi kwa mazoea.

Aidha, Dk. Mpango alimpongeza Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, kwa Kusimamia na kuwezesha urejeshwaji wa mali za Serikali, kupitia Kamati Maalum ya Uhakiki wa Mali za Serikali, ambazo zilikuwa zinamilikiwa na watu binafsi bila kufuata sheria na taratibu.