NA ABDI SHAMNA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) kuwekeza miradi yao nchini hususan katika sekta ya utalii.
Dk. Mwinyi alitoa wito huo jana ikulu jijini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Almarzouqi, aliyefika kujitambulisha kwa rais.
Alisema katika dhana ya kuimarisha uchumi, Zanzibar inalenga kuimarisha uchumi wake kupitia uchumi wa buluu, hivyo inahitaji wawekezaji kutoka mataifa mbali mbali duniani, ikiwemo UAE.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo muhimu la uwekezaji, hivyo akawataka wawekezaji kutoka nchi hizo kuja kuwekeza katika miradi mbali mbali.
Alisema sheria za uwekezaji, ikihusisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya miradi mbali mbali zinatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya visiwa.
Aidha, Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwa uhusiano mzuri na wa muda mrefu kati yake na Zanzibar na misaada mbali mbali inayoendelea kutolewa kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Alisema Umoja wa Falme za Kiarabu umekuwa ukiunga mkono juhudi za serikali na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, ambapo kwa nyakati tofauti zimesaidia miradi mbali, ukiwemo Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ unaolenga kuwawezesha kiuchumi vijana wa Zanzibar.
Vile vile aliziomba taasisi na wadau wa maendeleo kutoka nchi hizo kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuuweka katika mazingira bora zaidi Mji Mkongwe wa Zanzibar, (ulio katika Urithi wa Ulimwengu) ili uweze kuwa eneo la kiuchumi.
Naye, Balozi wa UAE nchini Tanzania Khalifa Abdulrahman Almarzouqi alimhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa UAE itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Zanzibar, sambamba na kuendelea kuisaidia nchi hiyo katika nyanja za Kiuchumi na kijamii.
Aidha, aliahidi kuwashajiisha Wawekezaji wa nchi hizo kuja nchini kuwekeza, akibainisha kuwepo kwa kampuni mbali mbali zinazowekeza katika sekta ya utalii kupitia miradi mbali mbali, ikiwemo ya ujenzi wa Hoteli kubwa za kitalii, michezo ya baharini na miradi mingineyo.